Mahakama ya Wilaya ya Temeke imeahirisha kwa mara ya nne kutoa uamuzi wa pingamizi la maombi ya kupitiwa upya kwa shauri la mirathi lililodumu kwa miaka 13.
Katika maombi hayo, mkazi wa Dar es Salaam, Khalfani Yusuph Shaweji ameiomba mahakama hiyo ifanye mapitio ya uamuzi wake wa Oktoba 2022 kwa madai kuwa ilikosea kisheria na ilipoamua kuwa faili la msingi la kesi ya mirathi halipatikani
Wiki iliyopita, aliyekuwa mke wa Shaweji, Sharifa Mohamed ambaye alipaza sauti kuuomba mhimili wa mahakama kuingilia kati shauri hilo ili liishe, akieleza kuchoka kwenda mahakamani kwa miaka 13 sasa.
Mwanamke huyo alifunguliwa shauri la mirathi katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mwaka 2011 akiomba talaka na kugawanywa kwa mali zilizochumwa ndani ya ndoa.
Mwaka 2014, mahakama hiyo ilikubaliana naye na kuzigawa mali za ndoa kwa uwiano wa asilimia 40 kwa Bi Sharifa na 60 kwa Shaweji.
Sharifa alipinga uamuzi huo akidai mali alizogawiwa hazikuwa zile alizoziainisha na kwamba hazikuwepo kabisa, hivyo alikata rufaa Mahakama Kuu akipinga mgawanyo huo.
Jaji Aloysius Mujulizi aliiondoa rufaa hiyo Mei 4 mwaka 2015 na kuamuru irudishwe Mahakama ya Wilaya ya Temeke na kusikilizwa upya mbele ya hakimu mwingine huku akiielekeza ijiridhishe kama ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza maombi hayo.
Mahakama ya Wilaya ya Temeke ilisikiliza tena shauri hilo na Novemba 10 mwaka 2016 ilikubali ombi la talaka na kuzigawa upya mali zilizochumwa kwenye ndoa kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50.
Kufuatia hukumu hiyo, Sharifa alianza utaratibu wa kukazia hukumu kwa kuthamini wa mali za ndoa na kutafuta dalali wa kutekeleza amri ya mahakama lakini harakati hizo zilikatishwa rufaa iliyokatwa na mume wake kupinga mgawanyo wa mali wa asilimia 50 kwa 50.
Jaji Ilvin Mugeta aliyesikiliza rufaa hiyo alianza kwa kuliitisha faili la kesi ya msingi ya talaka kupitia utaratibu wa kawaida wa mahakama lakini faili hilo halikupatikana hadi alipoamuru waleta maombi kufungua upya shauri katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke.
Kesi hiyo ilifunguliwa upya katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke na baada ya mahakama hiyo kujiridhisha kuwa nyaraka katika faili hilo zilikuwa zimechanganywa na nyingine hazipo, ilishauri amri ya Mahakama Kuu iheshimiwe na kuelekeza ikafunguliwe Mahakama ya Mwanzo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (One Stop Judicial Centre) Temeke.
Sharifa alifungua kesi hiyo na kupewa namba 1,479. Wakati kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi T. A Milanzi ikiendelea, upande wa pili walirudi tena Mahakama ya Wilaya ya Temeke kuomba kupitiwa upya kwa uamuzi uliolipeleka shauri hilo Mahakama ya Mwanzo.
Sharifa ameweka pingamizi dhidi ya maombi hayo ya mapitio akidai kushughulika na kesi hiyo ni kukiuka uamuzi wa Mahakama Kuu ulioifuta.
Ahirisho la nne
Kwa mara ya kwanza hakimu Milanzi aliahidi kutoa hukumu ya pingamizi hilo tarehe 13 Februari 2023 lakini ilipofika siku hiyo aliahirisha tena hadi tarehe 27 Februari 2023.
Nyaraka zinaonyesha kuwa ilipofika Februari 27 hakimu huyo hakutoa hukumu na kuahidi kuisoma tarehe 15 Machi 2023 lakini hakufanya hivyo kwa kuishia kutoa ahadi ya kuisoma hukumu hiyo Machi 24.
Ijumaa iliyopita (Machi 24) uamuzi iliahirishwa tena kwa mara ya nne huku hakimu akisema “kimsingi, hukumu yenu iko tayari, kuna nyaraka za muhimu kidogo kuhusu shauri hili bado nazitafuta lakini nawaahidi tarehe 31 hukumu itasomwa.”