Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyama yaibua jipya kwa wenye hoteli, maduka

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imeanza kutoza faini ya Sh20 milioni kwa kila kilo moja ya nyama iliyopita muda wake wa matumizi kwenye hoteli au maduka makubwa ya bidhaa maarufu kama supamaketi.

Faini hiyo ambayo mhusika anatakiwa kuilipa ndani ya saa 24 baada ya kukutwa na kosa ni sehemu ya operesheni inayoendeshwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukabiliana na bidhaa zilizopitwa na wakati au zinazoingizwa kwa njia za haramu. Bidhaa hizo ni nyama na zingine zitokanazo na maziwa.

Operesheni hiyo ilifahamika kwa mara ya kwanza kwa Chama cha Wamiliki wa Mahoteli (Hat), Desemba 13.

Kwa mujibu wa Imani Sichalwe ambaye anaongoza timu ya wakaguzi jijini Dar es Salaam, operesheni hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano na maofisa kutoka wizarani, polisi, Usalama wa Taifa, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

Alisema operesheni hiyo inalenga kukagua viwango na ubora wa nyama pamoja na bidhaa za maziwa ili kubaini kama kuna mojawapo hazipaswi kuwapo kisheria au zimeingizwa nchini bila kufuata sheria za nchi.

Hata hivyo, ofisa mtendaji mkuu wa Hat, Nura-Lisa Karamagi alisema operesheni hiyo inaendeshwa kiholela na hata faini inayolipishwa haitozwi kwa haki.

Alisema baadhi ya wanachama wao wamekaguliwa na miongoni mwao wamelipishwa faini ya kati ya Sh20 milioni hadi Sh200 milioni.

Hadi sasa hoteli ambazo zimekaguliwa ni City Plaza, Holiday Inn, Court Yard, Double Tree, Hyatt, Ilboru na Kibo Palace. Zingine ni Protea, Rivertrees, Serena, Southern Sun, Venus, Mount Meru Game Lodge, Mount Meru, New Africa na Village Supermarket.

Hata hivyo Mwananchi lifahamu kuwa ipo hoteli iliyokaguliwa na baadaye kuamuriwa kulipa kiasi kikubwa cha fedha kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya viwango vya ubora wa huduma.

Pia, Mwananchi limefanikiwa kuona nyaraka zinazoonyesha hoteli moja jijini Arusha iliyoamriwa kulipa faini ya Sh20 milioni kwa kilo ya nyama baada ya kukutwa nayo iliyokwisha muda wake. Hata hivyo haijulikani hoteli hiyo ilikuwa na kilo ngapi za nyama hiyo.

Akizungumzia ukaguzi unaofanywa, meneja msaidizi wa Holiday Inn Dar es Salaam, Christopher Mutandwa aliliambia Mwananchi kuwa timu ya wakaguzi ilifika hotelini kwake.

“Walikuja lakini tulikuwa safi, karibu bidhaa zetu zote zilikuwa hazina matatizo,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz