Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyama ya twiga yampeleka jela miaka 20

630c99ddd5a001abe73dd28581512a6f Nyama ya twiga yampeleka jela miaka 20

Thu, 15 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro imemhukumu mfanyabiashara Omari Bokoi kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya Sh milioni 333 baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na vipande vya nyama ya Twiga.

Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Helen Hoza alitoa hukumu hiyo, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi sita na vielelezo tisa vilivyowasilishwa mahakamani na upande wa mashitaka.

Mahakama iliwaachia huru washitakiwa wawili, Omari Mnoa na Peter Charles baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.

Katika mashitaka ilidaiwa mahakamani kuwa Oktoba 15 mwaka 2018 katika eneo la Muheza karibu na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi wilayani Same washitakiwa walikutwa na vipande vya nyama ya Twiga vyenye thamani ya Sh milioni 33.3 sawa na Dola 15,000 za Marekani.

Ilidaiwa pia kuwa Bokoi alikutwa na gunia moja likiwa na vipande hivyo ambavyo ni sawa na kuua twiga mmoja, akiwa amevibeba kwenye pikipiki aina ya Boxer yenye namba za usajili Mc 661 ATV, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwendesha mashitaka wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Samuel Magoka, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kufanya vitendo vya ujangili.

Alieleza kuwa, wanyama jamii ya twiga wameendelea kutoweka na serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kuwalinda.

Magoka alisema, twiga ni nembo ya taifa na kivutio cha watalii kinachoiingizia serikali fedha.

Kabla ya hukumu mshitakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana mke na mtoto ambao wanamtegemea na pia amekaa rumande kwa miaka miwili wakati wa usikilizwaji wa kesi yake.

Chanzo: habarileo.co.tz