Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Noti bandia za Sh500 milioni zanaswa Dar

89017 Notipic Noti bandia za Sh500 milioni zanaswa Dar

Wed, 18 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Noti bandia za thamani ya zaidi ya Sh500 milioni kama zingekuwa halisi, na mitambo ya kuzitengenezea zimekamatwa jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo limemfanya Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga kupendekeza adhabu kali kwa wanaohusika na vitendo hivyo.

Profesa Luoga alitoa mapendekezo hayo jana wakati wa kutoa taarifa ya kukamatwa kwa watu watatu wakazi wa Chanika waliokutwa na kiasi hicho cha fedha na mitambo.

Alisema kwa sasa adhabu ya kifungo inayotolewa ni ndogo ikilinganishwa na kosa lenyewe, akibainisha kuwa ipo haja ya kuanzisha majadiliano kuhakikisha adhabu dhidi ya wanaopatikana na makosa ya kutengeneza fedha haramu inakuwa kubwa.

“Kuna haja ya kuanza majadiliano kuhakikisha adhabu ya upatikanaji na utengenezaji wa fedha haramu inakuwa kubwa,” alisema.

“Suala la adhabu ni la mahakama, lakini kwa uhalifu wa namna hii ni mbaya na unahitaji adhabu ya kutosha itakayoendana na kosa lenyewe kwa kuwa zipo nchi zinazotoa adhabu ya kunyonga kwa makosa ya uhujumu uchumi,” alisema.

Profesa Luoga alibainisha kuwa tatizo ambalo nchi ilikuwa inakabiliana nalo si la kawaida. BoT ilichukua hatua kwa kulinda noti bandia zisiingie kwenye benki.

Alisema vyombo vya dola viliingia na kuhakikisha wanatambua mahali fedha haramu imetumika.

“Bila kuhakikisha uchumi unalindwa nchi inaweza kuhujumiwa. Moja ya hujuma ni fedha za kigeni kushambuliwa na hii hufanyika pale Benki Kuu inaposhindwa kuweka udhibiti,” alisema.

Luoga ametoa kauli hiyo zikiwa zimepita siku chache tangu wananchi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kusalimisha Sh700,000 bandia baada ya kutakiwa kufanya hivyo na mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, ambaye pia alikuwepo kwenye mkutano huo.

Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha imekuwa na matukio mengi ya kukamatwa kwa fedha bandia, jambo linalotajwa kuwa na athari katika uchumi wa nchi.

Kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema Benki Kuu ilitoa taarifa kwa polisi baada ya kupatikana kwa fedha bandia za Sh11 milioni wilayani Hai na kuanza msako katika wilaya zote za jiji la Dar es salaam.

Alisema Desemba 15, polisi kwa kushirikiana na wadau wengine walifanikiwa kumkamata mhalifu sugu ambaye amekuwa akijihusisha na kiwanda cha kutengeneza fedha bandia.

“Vitendo kama hivi vina madhara makubwa. Hatuwezi kuacha wahalifu kama hawa wakiharibu uchumi wa nchi yetu,” alisema Mambosasa.

Aliongeza kuwa katika msako huo miongoni mwa fedha bandia zilizokamatwa ni pamoja na dola, fedha za Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Sabaya aliyekuwepo katika mkutano huo alisema kwamba wiki chache zilizopita akikamata Sh11 milioni akibainisha kuwa waathirika wakubwa wa fedha bandia ni wajasiriamali wadogo.

Alisema wakishapokea fedha hizo wanaunganishwa na kutengeneza mfumo wa kughushi ukionyesha kwamba kuna fedha halali na uchumi halali ambao huathiri watu wenye uchumi wa chini.

“Kuna haja ya kuwa na adhabu kubwa inayoendana na kosa, watu hawa wamekuwa wakiathiri uchumi wa nchi hasa kwa wafanyabiashara wadogo,” alisema Sabaya.

Chanzo: mwananchi.co.tz