Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Nitumie kwa namba hii’ 11 watiwa hatiani, sita wafungwa

Simuuu ‘Nitumie kwa namba hii’ 11 watiwa hatiani, sita wafungwa

Fri, 29 Mar 2024 Chanzo: Mwananchi

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu wakazi 11 wa Ifakara, mkoani Morogoro, adhabu ya kulipa faini ya Sh6 milioni kila mmoja au kifungo cha miaka mitatu jela wakishindwa kulipa faini hiyo.

Mahakama imewahukumu adhabu hiyo baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutoa taarifa za uongo mtandaoni.

Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Fredrick Kanepela, Julius Mwabula, Amiry Luwiso, Tareeq Sadrudin, Ashraf Awadhi, Frank Kifyoga, Samson Tandike, Michael Haule, Mussa Maganga, Helman Lwambano na Kelvin Mkapila.

Hukumu ilitolewa Machi 26, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Annah Magutu baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka na kukiri makosa.

Walifanya hivyo baada ya kuingia kwenye majadiliano na kufikia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ya kumaliza kesi dhidi yao kwa kukiri makosa yao (plea bargaining).

Akisoma hukumu, Hakimu Magutu alisema imetolewa dhidi ya washtakiwa 11 pakee waliokiri makosa, kati ya washtakiwa 23 waliokuwa wanakabiliwa na kesi hiyo.

Awali, washtakiwa hao walisomewa mashtaka na jopo la mawakili wa Serikali Neema Moshi, Royda Mwakamele, Titus Aron, Cathbert Mbilingi na Winniwa Kassala.

Akiwasomea mashtaka, Wakili Moshi alidai washtakiwa wakiwa na nia ovu walitoa taarifa za uongo mtandaoni na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Alidai washtakiwa wanaojiita kwa jina maarufu 'Halo halo' walitoa taarifa za uongo wakitumia ujumbe usemao “nitumie hiyo hela kwenye namba hii.”

Alidai washtakiwa ambao walikamatwa kwa nyakati tofauti Ifakara, mkoani Morogoro, walikula njama na kutuma ujumbe wa kitapeli kwa nia ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutoa taarifa za uongo mitandaoni.

Imedaiwa washtakiwa wamekuwa wakiwatumia wananchi ujumbe wa maneno kwenye simu wa kitapeli na kupiga simu, huku wakidai wao ni wafanyakazi wa kampuni za simu na kuwatapeli wananchi fedha zao.

Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka walikiri kutenda makosa hayo ndipo Hakimu Maguta akawatia hatiani na kuwahukumu adhabu hiyo.

Watano kati ya waliokiri na kuhukumiwa adhabu hiyo waliweza kulipa faini ya Sh6 milioni kila mmoja na wakaachiwa huru. Wengine sita walipelekwa gerezani kuanza kutumia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu baada ya kushindwa kulipa faini.

Waliolipa faini na kuachiwa huru ni Fredrick Kanepela, Julius Mwabula, Amiry Luwiso, Tareeq Sadrudin na Ashraf Awadhi.

Walioshindwa kulipa faini na kupelekwa jela ni Frank Kifyoga, Samson Tandike, Michael Haule, Mussa Maganga, Helman Lwambano na Kelvin Mkapila.

Kesi imepangwa kuendelea Aprili 2, 2024 kwa washtakiwa wengine 12 waliosalia, ambao walikana mashtaka.

Chanzo: Mwananchi