Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni panga pangua kesi ya Mbowe na wenzake

Mbowepic Ni panga pangua kesi ya Mbowe na wenzake

Tue, 23 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Divisheni ya makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imetupilia mbali sababu tatu zilizowasilihwa na upande wa utetezi kwenye kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu ya kupinga kitabu cha kumbukumbu za watuhumiwa kupokelewa kama kielelezo.

Uamuzi huo wa mahakama ulitolewa jana mbele ya Jaji Joackim Tiganga, baada ya kupitia hoja za mawakili wa pande zote mbili waliokuwa wanalumbana kisheria kuhusu kitabu hicho cha kumbukumbu za watuhumiwa katika Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam (DR) kupokelewa ama la.

Kitabu hicho kilikuwa kinatolewa kama kielelezo wakati shahidi wa pili kwenye kesi ndogo, Koplo Msemwa alipokuwa akitoa ushahidi wake akieleza jinsi alivyowapokea mshtakiwa Adamu Kasekwa na Mohammed Ling'wenya Agosti 7, 2020 na kuwaweka mahabusu.

 

Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, walipinga na kutoa sababu tatu ikiwamo kukiukwa kwa taratibu za kutolewa kwa kielelezo hicho.

Akitoa uamuzi pamoja na mambo mengine Jaji Tiganga alisema mahakama inajiuliza jambo la kujadili DR lilikuwa linaifikisha mahakama mwisho ama la na jibu ni hapana.

Alisema kielelezo kinaweza kutolewa mahakamani kwa utambuzi, kinapokelewa kama utambuzi ni tofauti na kinapopokelewa kwa ushahidi na kinapopokelewa kwa utambuzi mahakama inakosa hadhi ya kukitumia kama kielelezo.

"Mahakama inaona suala la kutolewa kielelezo na shahidi halikuwa linaifikisha mwisho mahakama, mahakama inakuwa imefikia mwisho ikithibitisha kwamba jambo lililoko mbele yake limeshazungumzwa na kutolewa uamuzi, jambo hilo linatakiwa liwe limemaliza kesi kwa kumkuta mshtakiwa ana hatia au kuitisha jambo lolote, amri hiyo inatakiwa iwe na matokeo ya kufikisha kesi mwisho.

"Nazingatia hoja za pande zote mbili, hakuna ubishi kwamba DR ililetwa kwa utambuzi ikakataliwa sababu shahidi alishindwa kujenga msingi," alisema.

Jaji Tiganga alisema hoja iliyobakia ni kwamba kielelezo lazima kitoke kwa amri ya mahakama na imeelezwa bila kuwapo kwa amri hiyo utolewaji wa barua ya Naibu Msajili hakuwezi kuhalalisha suala hilo la utolewaji wa kielelezo.

Alisema mahakama inaona suala zima la upokelewaji wa kielelezo ni la kisheria, baada ya kielelezo kupokelewa kinabaki chini ya mahakama na kinapaswa kutolewa kwa amri ya mahakama.

"Nakubaliana na upande wa utetezi kwamba mahakama inapopokea kielelezo haihusiki na kutunza, kutunza ni jukumu la Hakimu Mfawidhi na Naibu Msajili.

"Amri inahusu kama kielelezo kinarudi kwa mwenyewe, kinaharibiwa au kinarudi serikalini, nakubaliana na upande wa utetezi kuwa Naibu Msajili hana mamlaka ya kutoa kielelezo, mamlaka yake ni kusimamia na pale kielelezo kinapokuwa katika chumba cha vielelezo.

"Kwa namna hiyo basi si kweli kwamba kielelezo hakiwezi kutolewa pasipo amri ya mahakama, hata hivyo mahakama inatakiwa ijielekeze katika sheria.

 

"Naibu Msajili ametajwa ana uwezo wa kutunza kielelezo kwa kesi zaidi ya moja au mahakama zaidi ya moja, kutokana na hali hiyo basi ni wazi sio kila wakati kielelezo kinapotakiwa kiwe na amri ya mahakama.

"Kielelezo kinaweza kutumika kwa kesi au mahakama zaidi ya moja bila amri ya mahakama, kielelezo sio lazima kitolewe kwa amri ya mahakama, Naibu Msajili ataandika katika kitabu cha kutoa kielelezo, kwa sababu hiyo natupilia mbali sababu zote tatu za kuzuia kupokelewa kwa DR," alisema na kupokea DR kama kielelezo cha upande wa mashtaka.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hillar, aliendelea kumhoji shahidi Koplo Msemwa ambaye alidai katika DR aliandika alivyowapokea watuhumiwa wawili kutoka kwa ACP Ramadhan Kingai na ASP Jumanne.

Alidai alimpokea Adamu Kasekwa na Mohammed Ling'wenya na aliwaingiza kwenye kitabu hicho saa 12.09 asubuhi Agosti 7, 2020.

Shahidi alipotakiwa kuwatambua watuhumiwa hao alidai wapo kizambani na aliwatambua kwa kuwaonyesha kidole.

Upande wa Jamhuri ulimaliza kuhoji maswali kwa shahidi huyo wa pili kwenye kesi ndogo ya kupinga maelezo ya Ling'wenya kupokelewa mahakamani kama kielelezo kwa madai aliteswa, alisainishwa maelezo ya onyo kwa vitisho na hakuwahi kufikishwa Kituo cha Polisi cha Kati kama inavyodaiwa na upande wa Jamhuri.

Mawakili wa utetezi walianza kumhoji shahidi kutokana na ushahidi wake, akihojiwa na Wakili Nashon Nkungu alidai Agosti 7, 2020 kituoni kulikuwa na askari wengine zaidi ya kina Kingai.

Alidai kuwa siku hiyo hakuna mtuhumiwa ambaye alitembelewa na ndugu yake.

Akihojiwa na Wakili John Mallya kuhusu sababu ya kumtoa mtuhumiwa mahabusu, shahidi alidai alimtoa kwa ajili ya masuala ya upelelezi na sio kwenda kumpiga kama anavyodai wakili.

Akihojiwa na Wakili Peter Kibatala, shahidi alikiri kwamba vitu vilivyochukuliwa kwenye diary yake vinahusiana na kesi na ushahidi wake aliotoa mahakamani.

Shahidi alidai hafahamu kama mahakama imechukua karatasi katika diary yake kabla hajaingia mahakamani kutoa ushahidi.

Akihojiwa kuhusu DR itatambulikaje kama ya Kituo cha Polisi cha Kati, Koplo Msemwa alidai ili kukitambua lazima kisomwe ndani kwa kuwa hakuna mahali kimeandikwa Kituo cha Polisi cha Kati.

Alidai wakati anampokea Ling'wenya hakumkuta na kitu chochote na kitabu cha kumbukumbu kiliacha kutumika tangu Agosti 12, 2020.

Alidai katika kitabu hicho Adamu Kasekwa alikuwa namba 393 na Ling'wenya alikuwa namba 392, alipotakiwa kusoma namba 208, shahidi alidai haisomeki.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbowe, Kasekwa, Ling'wenya na Halfani Bwire ambao wanakabiliwa na mashtaka sita likiwamo la kula njama kufanya vitendo vya kigaidi kati ya Mei mosi na Agosti 5, 2020.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live