Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni mauaji ya kusikitisha

19190 Mauaji+poic TanzaniaWeb

Tue, 25 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Muleba. Wakati mwanaume mmoja Kisiwa cha Ikuza wilayani hapa Mkoa wa Kagera akiuawa kwa madai ya kuchomwa kisu na mpenzi wake kwa madai ya wivu wa mapenzi, mauaji mengine yametokea maeneo mbalimbali nchini.

Miongoni mwa mauaji hayo ni kutoka Tabora ambako mtoto wa miaka minne amekutwa amekufa na mwili wake ukiwa umewekwa kwenye mfuko wa sandarusi.

Tukio jingine ni la wakazi wawili mkoani Geita ambao wameuawa kwa kukatwa mapanga na kunyofolewa sehemu mbalimbali za miili yao huku Mbeya mwanafunzi wa sekondari akitupa kichanga chooni baada ya kujifungua.

Katika tukio la wivu wa mapenzi lililotokea Muleba, Diwani wa Ikuza, Fortunatus Matha alimtaja aliyeuawa ni Masele Kalakiza (40) na aliyejeruhiwa ni Levina Gasper (38) ambaye amepelekwa Zahanati ya Kasenyi iliyopo kwenye kata hiyo.

Matha alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4:30 usiku katika Kitongoji cha Nyakaralo kilichopo Kijiji cha Ikuza eneo la Msenyi chanzo kikidaiwa ni wivu wa mapenzi.

“Mwanaume huyo ni mjasiriamali wa Kijiji cha Musonga kilichopo Kata ya Lunzewe wilayani Bukombe, ameuawa na mkewe, Maria Masele (28) kutokana na wivu wa mapenzi,” alisema Matha.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikuza, Lucas Kiberit alisema Maria alimfumania mume wake kichakani na kumchoma kisu upande wa kulia na utumbo kumwagika nje kabla ya kupoteza maisha.

Baada ya mauaji hayo, alisema Maria alikamatwa na uongozi wa kijiji na kukabidhiwa kwa askari wa kituo kidogo cha polisi kilichopo katika kisiwa jirani cha Kyakazimbwe ambao walimpeleka Kituo cha Polisi wilayani Muleba.

“Walikuwa kwenye starehe wanakunywa pombe ndipo mwanaume akachepuka kichakani na mwanamke mwingine; mkewe akamfuata kisha kumchoma kisu na kumjeruhi mwanamke aliyekuwa naye,” alisema Kiberiti.

Mwenyekiti huyo aliwashauri wananchi kulinda na kuthamini ndoa na familia zao kwa kuepuka kujichukulia sheria mkononi na inapotokea basi wapeleke mashauri yao kwenye mamlaka husika.

Mganga mfawidhi wa Zahanati ya Kasenyi inayomilikiwa na Kanisa la ELCT, Dk Martin Lujimya alisema majeruhi ameshonwa majeraha yake mkono wa kushoto na anaendelea na matibabu.

Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi cha Kyakazimbwe (OCS), Silasi Jeremiah alisema wanamshikilia mtuhumiwa na baada ya kuhojiwa atafikishwa mahakamani.

Aokotwa akiwa kwenye kiroba

Wakati wivu wa kimapenzi ukielezwa kutoa uhai wa mtu, mkoani Tabora, mtoto wa miaka minne Aisha Husseni alimeokotwa akiwa kwenye mfuko wa sandarusi akiwa amechomwa moto na watu wasiojulikana.

Tukio hilo lilitokea mtaa wa Sukuma juzi katika Kata ya Mbugani Manispaa ya Tabora.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley alisema uchunguzi unaendelea kufahamu nini kimetokea kwa mtoto huyo ili wahusika wakamatwe.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Hussein Maulid alisema walianza kumtafuta mtoto wao kuanzia Jumamosi iliyopita pasipo mafanikio na asubuhi ya juzi walielezwa wameuona mwili wa mwanaye ukiwa kwenye migomba.

“Tulimtafuta kila mahali na hatimaye kutoa taarifa kwa watu na kwenye msikiti kutangaziwa wananchi kuhusu kupotea kwake,” alisema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sukuma, Abdallah Salim alisema mtoto huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha na kukutwa ameuawa. Alivitaka vyombo vya dola kuhakikisha wahusika wote wanatafutwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa vile kitendo hicho hakikubaliki.

Wauawa, wanyofolewa viungo

Mkoani Geita, wakazi wawili wa Kijiji cha Lubanga wameuawa kwa kukatwa mapanga na kunyofolewa viungo mbalimbali vya mwili, tukio linalodaiwa kufanywa na watu wasiojulikana walioondoka na viungo hivyo.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Mponjoli Mwabulambo alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki na waliouawa ni mtu na shangazi yake ambao ni Kija Lushanga (70) na Pendo Bukelebe (48) na wauaji hao waliondoka na viungo hivyo.

Kufuatia mauaji hayo jeshi la polisi limewakamata watu wanne kwa mahojiano na uchunguzi bado unaendelea.

Kamanda huyo hakuwa tayari kuwataja wanaoshikiliwa kwa uchunguzi kwa kile alichodai kitaharibu uchunguzi.

Mwanafunzi amtupa mtoto chooni

Polisi mkoani Mbeya, linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha nne, Shule ya Sekondari Isengo kwa kosa la kumtupa chooni mtoto mchanga baada ya kujifungua.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei inasema tukio hilo limetokea jana asubuhi Mtaa wa Isengo, Kata ya Iyela, jijini humo.

Matei alisema mwanafunzi huyo alidaiwa kuwa mjamzito na baada ya kujifungua akatupa kichanga chooni. “Baada ya Jeshi la polisi kupata taarifa hiyo tulifika eneo la tukio, tulishirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na kufanikiwa kumuokoa mtoto huyo akiwa hai,” alisema.

Matei alisema mama na mtoto huyo wote wapo Hospitali ya Wazazi Meta jijini Mbeya wakipatiwa matibabu na kwamba upelelezi unaendelea na baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Wakati huohuo, Mkazi wa Kijiji cha Kasisi wilayani Chunya, Lutonja Lukelesha (33) amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu kwa mganga wa kienyeji baada ya kudaiwa kupigwa kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili na kukanyangwa kifuani kwa tuhuma za wizi.

Kamanda Matei alisema tukio hilo lililotokea Septemba 12, Lukelesha alituhumiwa kuiba redio ndogo yenye tamani ya Sh15,000.

Imeandikwa na Shaaban Ndyamukama (Muleba), Robert Kakwesi (Tabora), Rehema Matowo (Geita) na Ipyana Samson (Mbeya)

Chanzo: mwananchi.co.tz