Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema linaendelea na uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizotolewa na Askofu wa Kanisa la Efatha, Josephat Mwingira kuwa kuna njama za kumuua akiwahusisha viongozi wa serikali.
Akizungumza na HabariLEO jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro alibainisha kuwa uchunguzi wa undani wa suala hilo unaendelea huku akigoma kutoa maelezo ya kina kuhusiana na sakata hilo kwa kuogopa kuingilia uchunguzi.
HabariLEO ilipotaka kufahamu kama askofu huyo alifika mwenyewe kituoni kuhojiwa kama alivyoagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene kuwa ahojiwe ndani ya saa 24 na pia lilitaka kujua amehojiwa kwa saa ngapi, Kamanda Muliro alijibu:
“Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linaendelea vizuri na uchunguzi wa taarifa za Askofu Mwingira, taarifa hiyo inatosha, siwezi kuelezea kiundani kwani hairuhusiwi taarifa za kipelelezi kuzieleza hadharani, sielezi zaidi maana utaniuliza kama tumemuweka lockup au, hiyo inatosha ujue tu uchunguzi unaendelea vizuri sana.”
Kamanda Muliro alisema muda ukifika atazungumzia undani wa kile ambacho jeshi limekibaini.
Juzi Simbachawene aliliagiza jeshi hilo kumhoji Askofu Mwingira ndani ya saa 24 juu ya tuhuma mbalimbali alizozitoa dhidi ya serikali ikiwamo njama za maofisa wa serikali kutaka kumuua.
Waziri huyo alisema tuhuma zilizotolewa na askofu huyo ni nzito na haziwezi kuachwa bila kufanyiwa kazi hivyo wakati serikali inaendelea kuzifuatilia, ni vyema kiongozi huyo wa kiroho kujitokeza na kulisaidia Jeshi la Polisi ili ukweli uweze kujulikana.
“Tuhuma nzito kama hizo zinapotolewa na kiongozi ambaye ni wa kijamii katika dini na ni kiongozi ambaye ana umaarufu na anajulikana tunapata shida kidogo kwa sababu matukio yote haya kama ni kweli kama alivyosema ni kwanini hakutoa taarifa katika vyombo husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa kuwatafuta wahusika,” alihoji Simbachawene.
Alisema inatia mashaka kwa sababu mhusika aliyaacha mambo hayo yatokee tu mara kwa mara huku akisubiri ifike siku ya Krismasi ili aweze kutangaza hadharani katika nyumba za ibada na wakati huo wote alipokuwa anasubiri aliendelea kuwa salama bila kupata madhara.
“Kama aliyoyasema hayo ni kweli, basi tutahitaji atupatie maelezo na taarifa zaidi, kwa sababu tunafahamu kuwa yupo Dar es Salaam, si vibaya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu kumtafuta ili tuweze kupata maelezo yake zaidi kwa sababu tumesikia akizungumza na waumini wake lakini tunataka tumsikie ili tuweke katika rekodi,” aliongeza Simbachawene.
Alisema kwa kuwa Tanzania inaongozwa na utawala wa haki na sheria, mtu hawezi kukaa akiwa na hofu na maisha yake na pengine akaenda katika hatua kama alizozisema Askofu Mwingira na kuachwa kupita hivi hivi, hivyo kuna haja ya kupata maelezo zaidi.
Alisema baada ya Polisi Kanda Maalumu kuchukua maelezo ya kutosha hatua stahiki zitachukuliwa kwa wote watakaothibitika kujihusisha na njama hizo kama alivyoeleza Askofu Mwingira.
Hivi karibuni zilivuma taarifa katika mitandao ya kijamii zikimhusisha kiongozi wa huduma ya Efatha Ministries nchini Askofu Mwingira akisema alinusurika kuuawa mara tatu na watu kutoka serikalini na kwamba mali zake zenye thamani ya Sh bilioni 10 yakiwemo matrekta yaliteketezwa shambani kwake.
Katika madai yake Askofu Mwingira alidai kuwa dada aliyetoa taarifa za njama za kuuliwa kwake aliuawa katika Hoteli ya Rombo Shekilango mkoani Dar es Salaam ambapo dereva wake alihusishwa katika mauaji na alimnyang’anya simu baada ya kugundua mipango hiyo.