Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngoma nzito mlinzi anayedaiwa kubaka mtoto

Jela 1.jpeg Ngoma nzito mlinzi anayedaiwa kubaka mtoto

Sun, 23 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Mahakama ya Rufani Tanzania, imeamuru kusikilizwa upya kesi ya kubaka mtoto wa mwaka mmoja, inayomkabili Baraka Leonard, aliyekuwa mlinzi wa familia moja wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga.

Amedaiwa kutenda kosa hilo Agosti 10, 2017, saa mbili usiku alipoombwa na mfanyakazi wa ndani amsaidie kumbeba mtoto huyo ili aoshe vyombo, alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Hakuridhika na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, akakata rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga ambayo ilibariki kifungo hicho. Alikata tena rufaa Mahakama ya Rufani.

Pamoja na sababu nyingine saba za rufaa, ya kwanza, aliieleza Mahakama kuwa utaratibu wa kupanga hakimu wa kusikiliza shauri hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, haukuwa wa kisheria.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani Tanzania lililoketi mjini Shinyanga na kutoa hukumu juzi limekubaliana na hoja hiyo na kufuta hukumu hizo mbili na mwenendo wa kesi.

Hoja ya mrufani ni kama hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, E. N. Kyaruzi alikuwa na mamlaka ya kumpangia kesi hiyo hakimu wa mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga aitwaye R. S. Mushi.

Jopo la majaji hao, Augustine Mwarija, Ignas Kitusi na Agnes Mgeyekwa amesema mamlaka ya mahakama ya wilaya inaibana kushughulikia kesi za eneo hilo tu la kijiografia, labda tu kama ina mamlaka juu ya nyingine.

“Swali hapa ni je, hakimu mkazi mwandamizi Kyaruzi (wa Kahama) kumpangia hakimu mkazi Mushi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga hilo jalada ilikuwa ni sawa? Kama si sawa tunarekebishaje,’’ lilihoji jopo hilo.

Majaji hao walisema mrufani aliomba aachiwe moja kwa moja, lakini ili kuweka uwiano kati ya miaka aliyokaa gerezani na umri wa mtoto mdogo aliyeathirika, wanaamuru kesi isikilizwe upya.

Chanzo: Mwananchi