Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndugu washikilia msimamo kususia maiti Dar, polisi waeleza upya alivyouawa

13370 MAITI+PIC TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke imetoa ufafanuzi wa kifo cha Salum Kindamba ambaye ndugu zake wamegoma kuchukua mwili wake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa siku 12 sasa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula alisema jana kuwa mwili huo ulishafanyiwa uchunguzi na ndugu wanapaswa kuuchukua, akisisitiza kuwa alijeruhiwa kwa risasi katika tukio la uhalifu.

Lakini kauli hiyo haijabadili msimamo familia hiyo wa kutochukua mwili wa marehemu ikisema hata kama utakaa mochwari kwa miaka mitano, hadi jeshi hilo litakapoeleza ukweli ikiamini kuwa ndugu yao hakuwa jambazi.

Kamanda Lukula alisema mwili wa Salum ulifanyiwa uchunguzi na ndugu kukabidhiwa tangu Agosti 13, hivyo wanatakiwa kuuchukua.

“Mwili ulishafanyiwa uchunguzi na ndugu walikuwapo, lakini wameuacha hadi leo,” alisema.

Juzi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alikaririwa akiwataka ndugu hao kuchukua mwili huo kwa madai kuwa kuususia mochwari hakuwezi kubadili kitu, na ni kutoutendea haki.

Maelezo ya tukio

Kamanda Lukula alisema Agosti 11 walipokea taarifa kuwa katika eneo la Kiwalani Kigilagila kuna watu wanne waliokuwa na mfuko wenye silaha, hivyo walianza ufuatiliaji.

Alisema walipofika eneo la tukio waliwakuta watu hao na walipowafuata kwa ajili ya mahojiano mmoja alikimbia akiwa na mfuko huo.

Ili kurahisisha ukamataji, Lukula alisema askari walifyatua risasi tatu hewani asimame, lakini alikaidi na kusababisha risasi kumjeruhi mguuni na kiunoni.

“Polisi ilifanya kila jitihada za kufanikisha kumkamata mtuhumiwa lakini alikaidi. Kutokana na jeraha tulimpeleka Hospitali ya Temeke na alifariki (dunia) baadaye,” alisema.

Alisema upelelezi uliofanyika unaonyesha Salum alikuwa akijihusisha na vitendo vya uhalifu, ndiyo maana alikimbia na kukaidi amri ya polisi, hivyo kusababisha ajeruhiwe.

Aliwataja watu wengine waliokuwa na Salum kuwa ni Moses Halamela (30), Agape Mwakanyamale (34) na Omari Mhando (33) ambao walijisalimisha.

Kauli ya ndugu

Wakati polisi ikieleza hayo, familia ya Salum imeendelea kusisitiza kuwa haiko tayari kuchukua mwili ikieleza kuwa itaendelea kuususia mochwari hata kwa miaka mitano.

Msemaji wa familia hiyo, Omary Kindamba alisema jana kuwa polisi haitaki kusema ukweli kuhusu mauaji ya ndugu yao.

Alisema kutokana na utata uliopo, familia inahimiza kuundwa kwa tume huru itakayochunguza suala hilo. “Ndugu yetu hakuwa jambazi, siku ya tukio alikuwa ametoka kazini na wenzake watatu na kufika kwenye baa moja kwa ajili ya kupata chakula cha mchana, ghafla wakatokea watu watano wakawazingira, wakawamata na kuwapeleka katika gari tinted (vioo vya giza),” alidai Omary, “Wakati wanafanya hivyo hawakujitambulisha kama wao ni polisi... waliwapoka mfuko uliokuwa na fedha ndani yake kama milioni tisa.”

Omary alidai kwamba kutokana na mazingira hayo, ndugu yao aliwakimbia askari hao akidhani ni majambazi kwa kuwa hawakuonyesha vitambulisho wala kueleza kama walikuwa kwenye doria.

Alisema baada ya hapo askari hao walifyatua risasi na kusababisha kifo cha Salum.

Alisema ripoti ya awali ya polisi na ya Muhimbili ilionyesha kuwa alifariki kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali, lakini walipogoma kuipokea wamepewa nyingine inayoeleza alikufa kwa kupigwa risasi. “Hatuko tayari kuchukua mwili wa marehemu na hata ukikaa miaka mitano hatuko tayari mpaka jeshi hili litusafishe kwa maandishi kuwa ndugu yetu hakuwa jambazi na walimuua kwa bahati mbaya,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz