Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndugu waiachia dola ishughulikie kifo anayedaiwa kupigwa risasi na polisi

15455 Ndugu+pic TanzaniaWeb

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mafinga. Nelson Ngupula (31), mkazi wa mkoani Iringa anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi ubavuni na polisi eneo la Mafinga, Septemba Mosi, anatarajiwa kuzikwa kesho katika makaburi ya Mlowa, Iringa huku ndugu wakiililia dola.

Akizungumza na Mwananchi jana, mama mdogo wa Nelson, Siliva Kalinga alisema taarifa walizozipata zinaeleza kuwa aliondoka na rafiki yake aitwaye Onesmo Nzeru ambaye ndiye aliyekuwa akiendesha gari walilokuwa wakisafiria kwenda Mbeya.

Alisema wakiwa safarini walisimamishwa na askari wa usalama barabarani na kudaiwa kuwa na makosa mawili ambayo walitozwa faini ya Sh60,000 lakini dereva hakulipa na aliamua kuondoka.

Inadaiwa kuwa walipoondoka askari hao walitoa taarifa kwa wenzao waliokuwa kituo cha mbele gari lilikokuwa likielekea na walipowafikia na kusimamishwa, dereva huyo hakusimama ndipo wakaamua kulikimbiza gari hilo.

“Kwa taarifa alizozipata mdogo wangu ambaye alienda kuitambua maiti alisema aliambiwa kuwa baada ya kukaidi kusimama, mmoja wa askari aliamua kurusha jiwe akilenga kioo cha mbele, lakini hakufanikiwa ndipo wakapiga risasi kioo cha nyuma na kwenye tairi, lakini risasi iliyomuua Nelson inaonekana ilipigwa ubavuni lakini eneo la mlango alipokuwa amekaa haukuumia wala kutoboka,” alidai mama huyo mdogo.

“Inaonekana mpigaji risasi alipiga wakati mlango umefunguliwa kwa hiyo iliingilia ubavu wa kushoto ikatokea ubavu wa kulia, ikaingia kwenye mkono ikabaki mkononi.”

Alisema kutokana na kuonekana kuna utata juu ya kifo cha ndugu yao, waliomba mwili wake ufanyiwe uchunguzi kabla hawajauchukua ili kujiridhisha na sababu za kifo chake

Hata hivyo, alisema baada ya kuridhika na ripoti iliyotolewa na hospitali juu ya mazingira ya kifo hicho, ndugu wameamua kuuchukua mwili na kwenda kuuzika Iringa.

“Risasi zimeshatolewa mwilini mwa marehemu na Mungu akijalia tunausafirisha mwili leo (jana) na utaingia Iringa usiku na kesho (leo) tunatarajia kuuzika saa tisa,” alisema Siliva huku akisisitiza kuwa kwa sasa wameamua kuliacha suala hilo mikononi mwa vyombo vya dola.

Chanzo: mwananchi.co.tz