Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndugu wa watuhumiwa wa ugaidi waomba upelelezi uharakishwe

Kortinipic Data Ndugu wa watuhumiwa wa ugaidi waomba upelelezi uharakishwe

Thu, 17 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Familia za watuhumiwa watatu wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi katika Mahakama ya Wilaya ya Mtwara wameziomba mamlaka husika kuharakisha upelelezi ili haki na sheria zichukue mkondo wake.

Kesi hiyo namba tisa ya mwaka mwaka 2017 iliyopo chini ya hakimu, Musa Esanjo bado iko katika hatua ya kutajwa kwa vile upelelezi wake bado haujakamilika. 

Watuhumiwa hao ni mwalimu wa madrasa na mfanyabiashara mkazi wa Magomeni jijini Dar es salaam, Ramadhani Moshi Kakoso (44), fundi ujenzi mkazi wa Tandika na Waziri Suleiman Mkaliaganda (36) na mwalimu wa sekondari, mkazi wa Mtwara mjini, Omar Salum Bumbo (54).

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Februari 17, 2022 kaka wa mmoja wa watuhumiwa hao, Tiba Moshi Kakoso kwa niaba ya familia amesema wanaziomba mamlaka husika zikiwemo za uchunguzi kufanya kazi zao ili kama ndugu zao wana hatia basi sheria ichukue mkondo wake.

Amesema iwapo hakuna ushahidi wa kipelelezi kuhusiana na kesi hiyo basi haki itendeke ndugu zao hao waachiwe ili wakaungane na familia zao na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.

“Tunaomba vyombo husika vinavyosimamia haki viweze kuangalia shauri hili la ndugu zetu, ili haki ijulikane haki kama wana hatia au hawana, sisi kilio chetu ndio hicho hasa” alisema Kakoso.

Advertisement Amesema wamefanya jitihada kadhaa ikiwemo kuonana na Mkurugenzi wa Mashtaka ngazi ya mkoa hadi Taifa lakini majibu wanayoyapata ni kwamba suala hilo linashughulikiwa.

“Mkurugenzi wa Mashitaka aliyepita na huyu wa sasa walituambiwa kwamba kilio chetu wamekisikia na wanaomba tuwaamini tutulie tutapata majibu hivi karibuni” alisema Kakoso.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Musa Esanjo kuwa watuhumiwa hao walijiunga na kikundi kisichosajiliwa cha Hisbu Tahir ambacho shughuli yake ni kushawishi watu kujiunga na kutaka kuanzisha dola ya kiislamu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kesi hiyo inatarajia kutajwa tena mahakamani hapo Februari 23, 2022. 

Hata hivyo hivi karibuni, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Lugano Kasebele aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwa sasa ofisi ya mawakili wa Serikali makao makuu Dodoma wanashughulikia kesi za muda mrefu.

Kasebele aliongeza kuwa kesi za muda mrefu zinaweza kumalizika au kuanza kusikilizwa baada ya upelelezi na hatua nyingine za kimahakama kukamilika.

Katika kilele cha siku ya sheria duniani hivi karibuni mkoani hapa, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Zainab Muruke aliomba mamlaka zinazohusika na upelelezi kukamilisha taratibu za sheria ikiwa ni pamoja na kutoa vibali stahiki kesi zisikilizwe na kutolewa umauzi kwa wakati.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz