Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndugu wa marehemu tajiri wa madini wamkana anayedai mkewe

38787 Tajiri+pic Ndugu wa marehemu tajiri wa madini wamkana anayedai mkewe

Tue, 29 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ndugu wa marehemu katika kesi ya kugombea haki ya kumzika mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, Jubilate Ulomi wamemkana mke anayedai kuwa mke halali wa marehemu.

Kesi hiyo namba 4 ya mwaka 2019, imefunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Hai, Kilimanjaro na Zainabu Rashid ambaye aliyejitambulisha kuwa mke halali wa marehemu Ulomi, akidai haki ya kuuzika mwili wa mfanyabiashara huyo na uchunguzi wa kifo hicho.

Ulomi ambaye alikuwa mchimbaji na mmiliki wa migodi kadhaa ya madini ya Tanzanite huko Mirerani, alifariki dunia Januari 15 katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi Kenya.

Mazishi yake yaliyokuwa yamepangwa kufanyika mkoani Kilimanjaro hayakuweza kufanyika baada ya mwanamke huyo, Zainabu Rashid kufungua shauri hilo mahakamani kwa ushauri wa Mkuu wa Wilaya ya Hai kutokana na mgogoro uliowasilishwa kwake na kushindwa kupata mwafaka.

Hata hivyo, ndugu wa marehemu wamemkana mwanamke huyo kuwa hakuwa mke halali wa ndoa wa Ulomi.

Katika hati ya kiapo kinzani iliyowasilishwa mahakamani hapo Ijumaa iliyopita na mmoja wa walalamikiwa katika kesi hiyo, Onesy Ulomi amedai mwanamke huyo si mke halali kisheria na amemtaka athibishe madai hayo. “Jubilate Benjamin Ulomi alikuwa mdogo wangu na hakuwa na kwa uelewa wangu hakuwahi kufunga ndoa kisheria na mwombaji.”, anasema Onesy, katika hati hiyo ya kiapo kinzani, kilichowasilishwa mahakamani hapo na wakili Joseph Ngiloi na kuongeza:

“Jubilate alikuwa ametengana na kanisa lake kwa kuwa na watoto wengi na wanawake tofauti bila kufuata mwongozo wa kiroho, lakini aliungana tena katika kanisa lake baada ya toba mbele ya Mchungaji Chambulila wa Kaniasa la Good Samaritan na akasema kuwa hakuwahi kuwa na ndoa yoyote iliyosajiliwa.”

Mbali na Onesy, walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ni Werandumi Benjamin Ulomi, Awadi Ulomi na Abdulrasul Ulomi.

Mahakama ya Wilaya ya Hai imezuia ndugu wa marehemu kufanya mazishi wala kufanya chochote kuhusiana na mali za marehemu hadi shauri mama litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Katika maombi yake kwenye kesi hiyo iliyopangwa kutajwa mahakamani hapo Februari 7, Zainabu anadai kwamba alikuwa mke halali na wa kisheria wa Ulomi na kwamba waliishi pamoja kama mume na mke kwa miaka 12 na kupata watoto, wawili na kuwa walitengana kwa muda isivyo halali, lakini alibakia kuwa mke wa kisheria.



Chanzo: mwananchi.co.tz