Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndalichako ashtukia upigaji wa mamilioni

2DwkZl9koh4PNV5 Ndalichako ashtukia upigaji wa mamilioni

Tue, 20 Sep 2022 Chanzo: ippmedia

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako ameibua ubadhirifu wa mamilioni ya shilingi yaliyotolewa kutokana na fedha za mkopo wa UVIKO-19 kwa ajili ya ukarabati wa Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu Sabasaba.

Kufuatia ubadhirifu huo, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi katika chuo hicho kuangalia matumizi ya zaidi ya Sh. milioni 800 zilizotolewa kwa ajili ya ukarabati wa chuo.

Ubadhirifu alioubaini ni katika ununuzi wa vifaa vya ujenzi ambavyo vimenunuliwa kwa bei kubwa kuliko uhalisia, kuweka makadirio makubwa ya mahitaji ya vifaa vya ujenzi (BOQ) na kutopelekwa kwa baadhi ya vifaa katika chuo hicho wakati inaonyesha fedha zilishatolewa kwa ajili ya kuvinunua.

Prof. Ndalichako aliibua ubadhirifu huo baada ya kufanya ziara ya siku moja katika wilaya za Manyoni, Ikungi na Singida juzi kukagua miradi inayotekelezwa na serikali kupitia wizara yake.

"Hapa kuna vimelea vya ubadhirifu kwa sababu mtu ana malengo gani kuweka mifuko 2,900 ya saruji halafu hauleti chuoni? Kwa hiyo, suala hili lazima lipelekwe TAKUKURU lichunguzwe, haiwezekani vitu havijafika lakini fedha yote imeshatumika," aliagiza.

Prof. Ndalichako alitoa mchanganuo wa vitu ambavyo vina utata kuwa ni matofali yaliyokuwa yanatakiwa katika ujenzi ni 7,000 lakini kwenye BOQ waliandika 14,700 na fedha ilishatolewa.

Aliongeza kuwa bei ya saruji iliandikwa kuwa ni Sh.18,000 bila Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na pia kwenye BOQ iliandikwa itatumika mifuko 2,912 wakati inayotakiwa kwa ajili ya kazi hiyo ni mifuko 900 tu kwa mujibu wa mkandarasi, lakini fedha ilishatolewa ya mifuko 2,912.

Kuhusu nondo, waziri huyo alisema iliandikwa zinahitaji 1,198 lakini uhalisia zinazohitajika ni nondo 50 tu, lakini pesa iliyotolewa ya nondo 1,198 na bei iliyowekwa kwa nondo moja ni Sh. 8,000 badala ya Sh. 5,000.

Alisema vioo vimenunuliwa kwa Sh.120,000 lakini kwenye BOQ imeandikwa vimenunuliwa kwa Sh. 220,000, jambo ambalo linaondoa maana halisi ya kutumia 'force account' (mfumo wa kutumia nguvukazi ya ndani).

"Kwa ujumla kazi hii haifai hata kidogo, vitu havipo katika uhalisia kabisa na BOQ iliyotumika kwenda kuombea fedha haiwiani na jinsi vifaa vilivyonunuliwa, hapa itabidi watu wa ununuzi watusaidie. Je, huu mfumo wa 'force account' umezingatiwa?" alihoji.

Prof. Ndalichako alisema shida kubwa katika mradi huu vitu vya kununua viliwekwa vingi kuliko uhalisia, mfano vikiwekwa vifaa vya kuanzishia kazi kwamba yatanunuliwa mashoka 22, majembe 22, makoleo 22, nyundo 22 na matoroli 22 na fedha ilishatoka lakini hakuna hata kitu kimoja kilichotoka.

Pia alisema marumaru zinazohitajika kwa ajili ya kazi hiyo ni maboksi 900 lakini fedha iliyotoka ni ya maboksi 1,105 na pia bei ya mabati imeandikwa kuwa yamenunuliwa kwa Sh. 99,120 lakini chuo kilinunua kwa Sh. 60,000 tu.

Aliongeza kuwa katika mchanganuo wa gharama za ukarabati wa chuo hicho, ilikuwa ziletwe Sh. milioni 812 lakini zimeongezwa na kufikia Sh. milioni 862 na kwamba jambo hili halikubaliki.

"Rais amekuwa akisisitiza watendaji kuwa makini katika utendaji wetu kila senti ya serikali tuilinde, lakini hapa unauliza hakuna maelezo, kila unayemuuliza anasema 'sijui', sasa kwanini anayejua asingekuja atoe maelezo maana hii ziara yangu haikuwa ya kushtukiza," alisema.

Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu Sabasaba, Fatma Malenga, kila alipoulizwa na waziri kuhusu utata wa ununuzi wa vifaa hivyo, alisema mambo mengi yalikuwa yanafanywa na watu wa wizarani hivyo hajui lolote.

Chanzo: ippmedia