Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzoga wa swala wawaponza wawili Serengeti

11237 Pic+swala TanzaniaWeb

Fri, 10 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Wakazi wa kijiji cha Machochwe wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Daniel Wangwi (38) na Daniel Juma (16) wameburutwa mahakamani wakishtakiwa kwa makosa matatu ya uhujumu uchumi likiwemo la kukutwa na mzoga wa swala tomi mwenye thamani ya Sh1.1 milioni kinyume cha sheria.

Mwendesha mashtaka wa Jamhuri, Emmanuel Zumba ametaja mashtaka mengine yanayowakabili washtakiwa hao mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wilaya ya Serengeti, Ismael Ngaile kuwa ni kuingia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) bila kibali na kukutwa na silaha za jadi ikiwemo panga na kisu ndani ya hifadhi.

“Kwa pamoja washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo saa 5:30 usiku wa Agosti 6,” Zumba aliiambia mahakama jana Agosti 9, 2018.

Washtakiwa hao wamepelekwa mahabusu hadi Agosti 22 shauri hilo litakapotajwa tena.

Katika shauri lingine washtakiwa saba wanaodaiwa kukutwa na shehena ya vipande 290 vya nyamapori wameendelea kusota mahabusu licha ya dhamana yao kuwa wazi lakini walishindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwasilisha mahakamani fedha taslimu zaidi ya Sh29 ambayo ni nusu ya Sh58 milioni ya thamani ya nyara za Serikali wanayodaiwa kukutwa nayo kinyume cha sheria.

Washitakiwa wanaosota mahabusu tangu Agosti Mosi walipofikishwa mahakamani kwa kwa mara ya kwanza ni Joseph Nyambacha (41), na Tatu Machota (47), wote watumishi wa Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori (WMA) Ikona wilayani Serengeti.

Wengine ni Yohana Nyambeho (45), Peter Kongoli (38), Mayonga Hamisi (41), Jumatano Boniphace (35), Wangi Samweli (38), wote wakazi wa kijiji cha Bwitengi wilayani Serengeti.

Washtakiwa hao pia wanatakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye mali zisizohamishika zenye hati ambazo thamani yake imethibitishwa na mthamini wa Serikali.

Baada ya kushindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana, hakimu mkazi mfawidhi wilaya ya Serengeti, Ismael Ngaile anayesikiliza shauri hilo namba 74/2018 ameiahirisha shauri hilo hadi Agosti 15 litakapotajwa tena.

Chanzo: mwananchi.co.tz