Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzee wa miaka 65 adaiwa kumbaka mtoto wa miaka mitatu

25659 Mzee+pic TanzaniaWeb

Tue, 6 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mzee wa miaka 65, Mohamed Hassani anashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar es Salaam kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa miaka mitatu.

Wakati mzee huyo akitiwa mbaroni, Mahakama ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, imewahukumu kifungo cha miaka 30 jela wakazi wawili wa wilayani humo baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka kwa zamu, mwanafunzi wa darasa la tano.

Katika tukio la Dar es Salaam, mzee huyo ambaye anaishi Mburahati Motomoto anatuhumiwa kumfanyia vitendo hivyo mtoto huyo akiwa chumbani kwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Muliro alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 31.

“Taarifa za kubakwa mtoto huyo tunazo tunazishughulikia kwa mujibu wa sheria na tutahakikisha mtuhumiwa anafikishwa mahakamani,” alisema Muliro

Mama mlezi wa mtoto huyo, alisema siku ya tukio, mtuhumiwa alimwita mwanaye chumbani kwake ili amtume dukani, alimwandikia kwenye karatasi dawa ya Diclopar na pipi ili akanunue.

Alisema hawakuwa na wasiwasi naye kwa kuwa mtuhumiwa alikuwa mtu mzima na mara nyingi amekuwa akimwita mtoto huyo ndani kwake na wakati mwingine akimtuma.

Alisema kuwa mara nyingi mtoto huyo anapoingia ndani ya chumba cha mzee huyo anapotoka nje huwa anampa pipi, biskuti, juisi na vitu vingine vya kuchezea.

“Huyu mzee ni mpangaji mwenzetu, hana mke tulikuwa tunamheshimu sana wapangaji wote na tunamuita mjomba kutokana na uzee wake.

“Yaani sikuamini siku hiyo napigiwa simu na mpangaji mwenzangu akiniambia nirudi haraka nyumbani nikamwangalie mtoto amebakwa,” alisema.

Aliporudi alimkagua mtoto huyo na kubaini kuwa ameingiliwa kimwili ndipo akaenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Mburahati na kupewa fomu ya matibabu PF3 ili ampeleke Zahanati ya Mianzini.

Alisema alifungua jalada la kesi ya ubakaji yenye namba MBT/RB/5395/2018 na walienda kwenye zahanati hiyo lakini walipofika walielezwa na daktari kuwa hakuna vipimo vya kumpima mtoto huyo hivyo waende Hospitali ya Palestina iliyopo Sinza ambako daktari alimpima na kubaini ameingiliwa kwa sentimita 12 huku akiwaeleza kuwa amefanyiwa kitendo hicho kwa muda mrefu.

Alisema daktari huyo alimpima ili kuangalia kama ameambukizwa virusi vya Ukimwi na alimwandikia dawa za mwezi mmoja kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa ripoti za matukio ya ubakaji iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kati ya Januari hadi Juni, watoto 2,365 wamebakwa na kila mwezi watoto 394 wanabakwa

Kutoka Hai

Rashidi Abdu (21), mkazi wa Kijiji cha Miaseni na Agustino Seki (21) wa Kijiji cha Sadala wilayani humo wamehukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa kosa la ubakaji.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Hai, Devotha Msofe baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi wanane wa upande wa mashtaka.

Awali, ilidaiwa na Mwendesha mashtaka, Hawa Hamisi kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Oktoba, 2016 na kumsababishia maumivu mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 12.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwendesha mashtaka aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kutokana na kile alichodai vitendo vya ubakaji hasa wanafunzi vinazidi kuongezeka nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz