Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzee wa miaka 64 kizimbani kwa tuhuma kujifanya Polisi

KIZIMBANI 2 Mzee wa miaka 64 kizimbani kwa tuhuma kujifanya Polisi

Tue, 10 May 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mkazi wa Bahi jijini Dodoma, Dominick Bruno (64) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Igunga kwa tuhuma mbili ikiwAmo ya kujifanya ofisa wa Jeshi la Polisi.

Mwendesha mashtaka wa Polisi Wilaya ya Igunga, Ellymajid Kweyamba ameiambia mahakama mbele ya hakimu wa Wilaya ya Igunga, Lydia Ilunda, kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na makosa mawili.

Katika kosa la kwanza, ameeleza mahakama kuwa Februari 3, 2022  katika Kijiji cha Igurubi na Kata ya Igurubi Wilaya ya Igunga Mkoa wa Tabora, mshtakiwa huku akitambua kuwa ni kosa alijitambulisha kwa ndugu Masunga Masesa mkazi wa Kijiji cha Igurubi kuwa yeye ni ofisa wa upelelezi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma.

Aliendelea kuiambia mahakama kuwa mshtakiwa huyo, ametenda kosa hilo kinyume na kifungu 100(b) kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho Mwaka 2019.

Amesema shtaka la pili kwa mshtakiwa ni kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kinyume na na kifungu 301 na 302 kanuni ya adhabu sura ya 16 marekebisho ya mwaka 2019.

Ameeleza kuwa katika tarehe tofauti Februari 3, 2022 na Machi 8, 2022 katika Kijiji cha Igurubi kwa njia ya udanganyifu alijipatia fedha taslimu Sh4 milioni kutoka kwa Masunga Masesa ambapo alijitambulisha kuwa yeye ni mkuu wa upelelezi Mkoa wa Dodoma ambapo alitaka kiasi hicho cha pesa ili asimkamate kwa tuhuma ya mauaji.

Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa alikana kutenda makosa hayo mawili ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 20, 2022 na mshitakiwa amepelekwa mahabusu baada ya kukosa mdhamini kwani alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja wa kusaini dhamana ya Sh2 milioni.

Mwendesha mashitaka huyo ameiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz