Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzee wa miaka 61 jela maisha kwa kumbaka mtoto wa miaka minane

HUKUMU Mzee wa miaka 61 jela maisha kwa kumbaka mtoto wa miaka minane

Thu, 21 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, imemhukumu kifungo cha maisha gerezani, Christopher Mariki (61) baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka minane.

Mariki ambaye ni mkulima na mkazi wa Kijiji cha Imbaseni wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, amehukumiwa adhabu hiyo na Hakimu Mkazi Itikija Nguvava, baada ya kumtia hatiani kwa kosa hilo la kumbaka mtoto huyo kwa nyakati tofauti.

Akisoma hukumu hiyo leo Alhamisi Septemba 21, 2023, hakimu huyo amesema mahakama imemtia hatiani mtuhumiwa huyo aliyekuwa anakabiliwa na kosa la ubakaji.

Amesema katika kesi hiyo ya jinai namba 38/2023 upande wa jamhuri umeweza kuthibitisha kosa hilo pasipo na shaka kupitia mashahidi wake wanne na mtuhumiwa huyo kuthibitika kumbaka mtoto huyo.

"Kutokana na ushahidi wa upande wa mashtaka ulionyesha mshtakiwa alikuwa na tabia ya kumbaka mara kwa mara mwathirika na hilo lilithibitishwa na mashahidi waliotoa ushahidi mahakamani na mahakama imeridhika kesi dhidi ya mshtakiwa imethibitishwa bila kuacha shaka lolote hivyo mahakama imemtia hatiani mshtakiwa na kumpa adhabu ya kifungo cha maisha jela," amesema.

Upande wa jamhuri katika kesi hiyo uliwakilishwa na mawakili wanne wakiongozwa na Wakili wa Serikali Grace Madikenya, ambaye amedai mahakamani hapo kuwa Machi 4, 2023 alimkuta mwathirika akiwa anachunga mbuzi, ambapo alimchukua na kumpeleka kichakani na kumbaka, ambapo aliendelea kufanya kitendo hicho kwa nyakati tofauti.

Awali Wakili Grace aliomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa huyo ili iwe fundisho kwa jamii.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live