Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwili wa kichanga waokotwa kwenye taka

Thu, 14 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Mwili wa kichanga umeokotwa leo Jumatano Februari 13, 2019 kando ya rundo la taka mtaa wa Manga B kata ya Manga jijini Mbeya.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Manga iliyopo jirani na eneo hilo ndio waliobaini mwili wa kichanga hicho.

Tabia Mwinuka, mkazi wa eneo hilo amesema wanafunzi ndio walioona mwili wa  mtoto huyo saa 2 asubuhi  wakati wakielekea shuleni.

"Wanafunzi waliona nguo za kuvutia ambazo mwili wa mtoto huyo ulikuwa umezungushiwa, wakati wakishangaa mama mmoja alipowaona wakishangaa waliwafuata na kubaini mwili wa mtoto huyo,” amesema Tabia.

Ofisa mtendaji wa mtaa huo, Furaha Mlelwa amesema alipokea taarifa kutoka kwa wakazi wa eneo hilo na kutoa taarifa polisi.

"Mpaka sasa hatujajua aliyefanya tukio hilo ni nani tunawaachia polisi wafanye kazi yao," amesema Mlelwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,  Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kuwa mtoto huyo alikutwa ameshafariki dunia.

“Kuna alama zinaonyesha mtoto alikuwa kituo fulani cha afya hivyo tunaendelea kufuatilia ikiwa ni pamoja na kumbaini aliyefanya tukio hilo," amesema Matei.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz