Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwenyekiti wa kitongoji aharibu sehemu za siri za mkazi

7039220abb6b3feb1b2866a55f1c60d7.png Mwenyekiti wa kitongoji aharibu sehemu za siri za mkazi

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MWENYEKITI wa Kitongoji cha Maretoni kata ya King'ori wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha, Juma Bulele ametoa kali ya mwaka baada ya kumtembezea kichapo kikali mkazi wa eneo hilo na kuharibu sehemu za siri kwa kuzibondabonda.

Bulele ambaye kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha alimshambulia vikali mkazi wa eneo hilo aliyetambuliwa kwa jina la Edward Msemakweli(26) na kumsababishia maumivu makali sehemu za siri mara baada ya kumkuta akizungumza na simu usiku.

Akizungumza kwa shida, Msemakweli alisema kuwa tukio hilo limetokea katika kitongoji hicho Novemba 25, mwaka huu, saa tano usiku, baada ya mwenyekiti huyo kumkuta akizungumza na simu na kuchukua jiwe na kuanza kumshambulia sehemu za siri.

Msemakweli ambaye ni fundi ujenzi, amelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mount Meru baada ya kufanyiwa operesheni ya utumbo na sehemu za siri zililokuwa zimesagika kutokana na kupondwa na jiwe na Mwenyekiti huyo.

Alisema kuwa siku ya tukio alitoka nyumbani kwake majira ya usiku na kwenda kununua vocha ili aweze kuwasiliana na fundi mwenzake kwa ajili ya kumpatia vifaa vya ujenzi ili kesho yake aweze kuamkia kibaruani.

Alifafanua kwamba akiwa anaongea na simu kando kidogo na eneo la duka, ghafla alitokea Mwenyekiti Bulele na kumuuliza kwanini unaongea na simu muda huu usiku ukiwa peke yako.

Alisema Mwenyekiti huyo ambaye alionekana kuwa katika hali ya ulevi aliokota jiwe na kuanza kumshambulia kwa kumpiga tumboni mara kadhaa na kuanguka chini ambapo alianza kumpiga na jiwe hilo sehemu za siri jambo lililofanya apoteze fahamu.

"Baada ya kunipiga nilisikia maumivu makali sana na kuanguka chini na kupoteza fahamu na baadaye nilizinduka na kujikuta nipo katika hospitali nimelazwa sikujua kilichoendelea ,"lisema Msemakweli

Kwa upande wa mke wa majeruhi, Logati Jonathan alisema kuwa siku ya tukio mumewe aliondoka nyumbani usiku kwenda kununua vocha alishangaa kusikia alivamiwa na Mwenyekiti wa kitongoji na kushambulia hadi kupoteza fahamu.

"Hili tukio limenisikitisha sana kwani mume wangu ndio namtegemea kwa kila kitu hivi sasa hatuna chakula, watoto wanalala na njaa hatuelewi tufanye nini tunaomba serikali ichukue hatua kali kwa huyu mhusika,"alisema

Naye, baba mkwe wa majeruhi Jonathan Palangyo anayemuuguza majeruhi huyo alidai kwamba, maelezo ya daktari yanaonyesha aliumia sehemu ya tumbo na utumbo mpana kukatika pia sehemu za siri zilisagika hivyo uwezekano wa kuzaa utakuwa mdogo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Salumu Hamduni alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akidai kwamba mtuhumiwa anashikiliwa na uchunguzi unafanyika na punde atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.

Chanzo: habarileo.co.tz