Dodoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma imemkamata mwenyekiti baraza la ardhi la kata ya Makutupora mjini Dodoma, Petro Sengula (55) kwa madai ya kuomba rushwa ya Sh500,000 na kupokea Sh100,000.
Mwenyekiti huyo alikamatwa jana Jumatatu Septemba 30, 2019 akidaiwa kuomba rushwa kutoka kwa mwananchi aliyekuwa na shauri la mgogoro wa ardhi katika baraza hilo.
Akizungumza leo Jumanne Oktoba Mosi, 2019 mkuu wa taasisi hiyo Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo amewaeleza waandishi wa habari kuwa mtuhumiwa huyo wamefanya kosa kinyume na kifungu cha 15 (1) a cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sura ya 329 marejeo ya mwaka 2018.
Kibwengo amesema baada ya kupata taarifa walifuatilia na kujiridhisha kwamba ni kweli mtuhumiwa aliomba fedha hiyo ili amsaidie mtoa taarifa .
“Ndipo tukaweka mtego wa kumnasa katika eneo la Veyula kata ya Makutupora na kufanikiwa, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya taratibu za uchunguzi kukamilika,” amesema Kibwengo.