Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwandishi wa habari jela miezi minane kwa rushwa

2a9d299e7459c9800bf99c3412a3ee8e Mwandishi wa habari jela miezi minane kwa rushwa

Thu, 26 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara imemhukumu mwandishi wa habari wa kujitegemea, Patrick Chambo kwenda jela miezi minane baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Victor Kimario alitoa hukumu hiyo jana wakati mshitakiwa akiwa hayupo mahakamani na waendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Martin Makani na Evalyine Onditi kuiomba Mahakama itoe hukumu kali kwa mshitakiwa kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.

Awali katika hati ya mashitaka ilidaiwa kuwa, mshitakiwa alifanya kosa ambalo ni kinyume cha kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Manyara Holle Makungu alidai Chambo aliruka dhamana ya Mahakama baada ushahidi kukamilika na ukatolewa uamuzi mdogo kwamba alikuwa na kesi ya kujibu.

Alisema badala mshitakiwa kujitetea aliruka dhamana na kujinyima haki ya kusikilizwa na kuomba itolewe hati ya kumkamata ili atumikie hukumu hiyo.

Makungu alisema awali Chambo alifikishwa mahakamani akishitakiwa kwa makosa ya kuomba rushwa ya Sh 300,000 kwa mkurugenzi wa kiwanda cha vinywaji vikali ya Mati Super Brands Limited kilichopo mjini Babati mkoani Manyara.

Takukuru ilidai mshitakiwa alipokea Sh 150,000 ikiwa ni sehemu ya kiasi alichohitaji.

"Kwa mujibu wa uchunguzi wetu Chambo aliomba rushwa hiyo kwa maelezo kwamba alikuwa na ushahidi wa kutosha kuwa kiwanda hicho kilikuwa kikikwepa kodi ya serikali hivyo endapo wasingempa rushwa hiyo angewaaandika kwenye vyombo vya habari," alidai Makungu.

Alidai baada ya kampuni hiyo kuwasilisha malalamiko kwenye taasisi hiyo yalifanyiwa kazi na kuwezesha kukamatwa kwa Chambo akiwa amepokea rushwa hiyo.

Alisema uchunguzi wa Takukuru kuhusu kampuni hiyo ulibaini kuwa ni kweli ilikuwa imekwepa kodi ya zaidi ya Sh milioni 5.

"Tumeitaka kampuni hiyo kuhakikisha inalipa kodi hiyo pamoja na faini ya Sh milioni 50 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na tunaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya ulipaji wa kodi za serikali kwa kampuni hiyo ili kuhakikisha mapato halali ya serikali hayahujumiwi," alisema Makungu.

Chanzo: habarileo.co.tz