Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanamke wa kumi auawa Mto wa Mbu

53622 Pic+mwanamke

Tue, 23 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mji wa Mto wa Mbu uliopo wilayani Monduli umehesabu tukio la kumi la kuuawa kwa wanawake katika mazingira ya kutatanisha, safari hii Anastazia Paulo (62), akikutwa amefariki dunia katika nyumba aliyokuwa anaishi.

Tukio hilo ni la kumi kwa wanawake kuuawa ndani ya miaka mitatu katika mazingira ya kutatanisha yanayohusishwa na imani za kishirikina, ulevi, wivu wa mapenzi na ukatili wa kijinsia.

Machi 2, Ester Fisso (26) alibakwa kisha kuuawa kikatili.

Mbali na Ester wanawake wengine waliouawa kwa nyakati tofauti na kutambuliwa ni Ruth Elias, Vick Kivuyo, Elizaberth Hango, Shikweshi Boaz, Mwapwani Mawezo na Khadija Raphael.

Wakizungumza na Mwananchi, jana, baadhi ya majirani wa nyumba aliyokuwa akiishi Anastazia walisema juzi baada ya kutomuona walitilia shaka na kuamua kuvunja mlango uliokuwa umefungwa.

“Hatujui nini chanzo cha kifo, lakini tumekuta mwili ndani na mlango ulikuwa umefungwa kwa nje,” alisema Mariam Athuman, mmoja wa majirani.

“Mlango ulipovunjwa mwili wake ulikutwa tayari umeanza kuharibika na tulitoa taarifa polisi, wakafika na kuanza uchunguzi wao.”

Mariam alisema Anastazia ambaye alikuwa akiishi peke yake ameacha watoto wanane na mwili wake ulizikwa jana baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Jonathan Shana alisema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho.

Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa matukio ya uhalifu katika mji wa Mto wa Mbu huku akionya kuwa yeyote anayehusika ajisalimishe mwenyewe.

“Kuna maofisa wanaendelea na uchunguzi Mto wa Mbu kuhakikisha wote wanaohusika na uhalifu tunawakamata, tayari tumekamata watuhumiwa kadhaa ila bado uchunguzi unaendelea kujua kama wanahusika ama la.”

Mwezi Februari, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alifanya ziara katika mji huo na kupokea malalamiko ya wanawake waliotaka wahusika wa mauaji wasakwe na kukamatwa.

“RPC leta hapa kikosi cha intellijenjia wakae hapa kuhakikisha wanakusanya taarifa za wahalifu na kuwakamata,” aliagiza Lugola.



Chanzo: mwananchi.co.tz