Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanamke mwingine auawa Mto wa Mbu, mwili watelekezwa

40533 Mwanamke+pic Mwanamke mwingine auawa Mto wa Mbu, mwili watelekezwa

Thu, 7 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Matukio ya kuua wanawake baada ya kufanyiwa ukatili, yameibuka tena katika eneo la Mto wa Mbu wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha, baada ya Ester Fisso (26), kuuawa na mwili wake kutelekezwa eneo la Comwex.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Longinus Tibishubwamu alisema jana kwamba polisi wanafanya uchunguzi wa tukio hilo.

“Baada ya kupata taarifa kamili nitazitoa,” alisema Tibishubwamu.

Ester ni mtoto wa Mchungaji Philipo Fisso wa Kanisa la Elim Pentekoste Mto wa Mbu.

Kifo cha mwanamke huyo kinafikisha jumla ya wanawake tisa ambao wamekutwa wameuawa katika mazingira yanayofanana kwenye eneo hilo kwa takribani miaka minne sasa.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kwa nyakati tofauti mwaka jana, walitembelea mji huo baada ya kutokea mauaji ya wanawake na kutangaza mkakati wa kudhibiti matukio hayo na kuagiza kuimarishwa kwa ulinzi wa doria.

Licha ya ulinzi wa polisi, watendaji wa mitaa katika mji huo walianzisha ulinzi shirikishi wa usiku unaodaiwa kuwa ulifanikisha kudhibiti matukio ya uhalifu katika mji huo ambao ni maarufu kwa kilimo cha ndizi.

Akizungumza na Mwananchi juzi, Mchungaji Fisso alisema kifo cha mtoto wake kimemsikitisha kwa sababu umri wake ulikuwa bado mdogo na ameacha watoto wawili wadogo.

Mwili wa Ester ulionekana juzi asubuhi katika shamba la migomba ukiwa umetupwa huku ukiwa na majeraha kadhaa. Mmoja wa mashuhuda, Ally Yahaya alisema ulibainika baada ya watu waliokuwa wanapita njia asubuhi kuuona ukiwa umetupwa.

“Inaonekana ameuawa sehemu nyingine wauaji wakaja kuutupa mwili wake pale kwa sababu kulikuwa hakuna dalili za purukushani katika eneo hilo,” alisema Yahaya.

Mchungaji Fisso alisema mwili wa binti yake huyo ulitarajiwa kufanyiwa uchunguzi jana ili kubaini chanzo cha kifo chake, licha ya kwamba ulikuwa na majeraha mengi na ulikuwa ukivuja damu katika sehemu mbalimbali.



Chanzo: mwananchi.co.tz