Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanajeshi mbaroni tuhuma za ujambazi

45570 Pic+mwanajeshi Mwanajeshi mbaroni tuhuma za ujambazi

Sat, 9 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa wanne wa ujambazi akiwamo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kamanda wa polisi kanda hiyo, Lazaro Mambosasa jana alisema tukio hilo lilitokea Machi 3 mwaka huu na kwamba askari huyo wa JWTZ alikiri kumiliki silaha mbili na kuzitumia kwenye matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es salaam na Pwani.

Alisema wakati akihojiwa, askari huyo aliwaambia polisi kuwa alikuwa akizihifadhi silaha hizo nyumbani kwa mke wake mdogo mkoani Pwani.

Kamanda Mambosasa alisema polisi walifika kwenye nyumba hiyo na kukamata silaha aina ya AK 47 yenye namba NM 174844 ikiwa na risasi 20, boksi lenye risasi 27 na bastola yenye namba 3249 ikiwa na risasi saba na risasi nyingine tatu za silaha ya G3.

“Mtuhumiwa alikubali kuwaonyesha polisi wenzake watatu anaoshirikiana nao, askari walipofika kwenye nyumba wanayoishi walianza kukimbia kupitia mlango wa nyuma. Hilo liliwafanya askari warushe risasi hewani kuwaamuru wasimame lakini wakakaidi ndipo walipowafyatulia risasi ambazo ziliwajeruhi na walifariki wakiwa njiani kupelekwa hospitali,” alisema.

Katika hatua nyingine Mambosasa amegoma kuzungumzia kauli iliyotolewa na Rais John Magufuli kuhusu polisi kutoweka wazi baadhi ya mambo katika sakata la kutekwa na kupatina kwa mfanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji.

Akiwaapisha mawaziri Machi 4, Rais Magufuli alisema kuna kasoro katika utendaji wa Jeshi la Polisi, akiwatahadharisha kuwa Watanzania si wajinga wanahoji masuala mengi, akitoa mfano wa sakata la kutekwa kwa Dewji kwamba limeacha maswali mengi ambayo yanahitaji majibu.

Mambosasa alijibu kwa kifupi: “Nilishaliongelea hilo hivyo sipaswi kuongea chochote, aliyeongea ni amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, alitoa maelekezo na sie tumefundishwa amiri jeshi akiongea huwa hakuna majadiliano hakuna ufafanuzi.”



Chanzo: mwananchi.co.tz