Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi sekondari afariki kwa kuchomwa kisu kifuani

Polis Polis Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi, Ronald Makona

Fri, 27 Aug 2021 Chanzo: Ippmedia

Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Rau iliyoko Manispaa ya Moshi, Joachim Sanga, amefariki baada ya kuchomwa kisu kifuani katika ugomvi ambao chanzo chake bado hakijajulikana.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi, Ronald Makona, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba Sanga alifikwa na umauti juzi baada ya kuvuja damu nyingi.

“Ni kweli hilo tukio la mauaji lilitokea juzi saa 11 jioni huko katika viwanja vya Shule ya Sekondari Rau, wakati wanafunzi hao wakicheza mpira. Uchunguzi wetu wa awali unaonyesha kulikuwa na ugomvi wa kudaiana fedha walizokopeshana.

“Inasemekana kwamba marehemu na mtu mwingine ambaye si mwanafunzi walikuwa wakidaiana, ndipo waliposhindwa kuelewana na mmoja kumchoma mwenzie kisu kifuani.

“Baada ya tukio hilo, Sanga alikimbizwa Hospitali ya Rufani ya KCMC kwa ajili ya matibabu, lakini amefariki dunia muda mfupi baada ya kuanza kupatiwa matibabu.”

Kutokana na mauaji hayo, Kamanda Makona, amesema Polisi inamsaka mtuhumiwa wa mauaji hayo ambaye alitoroka na kukimbilia kusikojulikana.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Said Mtanda, amesema marehemu alichomwa kisu na kijana mwenzake ambaye alihitimu shuleni hapo miaka ya nyuma.

Mkuu wa Shule hiyo, Agustino Sanga, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, amesema marehemu alifikwa na mauti hayo, wakati wanafunzi wa shule yake na Shule ya Sekondari Karanga wakichuana katika mpira wa miguu.

Chanzo: Ippmedia