Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi auawa kwa kipigo cha mwalimu

Enock Kipkoech Mwanafunzi auawa kwa kipigo cha mwalimu

Wed, 5 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Familia moja mjini Eldoret nchini Kenya, imetaka haki itendeke kufuatia mtoto wao Enock Kipkoech, mwenye umri wa miaka 14, kupatikana amefarikia katika bweni la Shule ya Msingi ya St Teresa, katika Kaunti ya Kericho.

Kutokana na taarifa ya familia hiyo, Enock Kipkoech aliripoti kwa muhula wa tatu katika Shule ya Msingi ya St Teresa mnamo Jumatatu, Septemba 26, akiwa buheri wa afya.

Kwa mujibu wa ripoti ya K24, familia ya Enock inasema mwili wa marehemu ulikutwa na majeraha mabaya mwilini mwake baada ya kupigwa vibaya huku ikidaiwa kuwa alifanyiwa unyama huo na mmoja wa walimu wake.

“Kipkoech aliambiwa ahame kutoka kwa darasa lake wakifanya mitihani yao lakini baadaye alirudisha dawati lake darasani baada ya mitihani hiyo, hatua iliyomkasirisha mwalimu wake aliyemtaka aende kwenye ofisi ya walimu ambako alishushia kipigo kizito.

"Baadhi ya wanafunzi walisikia kilio chake cha uchungu akitokea kwa chumba cha walimu. Kisha mwalimu huyo alimfuata darasani na kumwagiza aende moja kwa moja hadi bwenini na kuoga.

"Hapo ndipo alipopatikana akiwa amefariki majira ya saa 4:00 jioni akiwa amening’inia kwa kujitia kitanzi,” babake mvulana huyo Richard Siele alisema.

Mama yake mvulana Emily Siele alisema mwanaye alikuwa ameomba shule imruhusu kumpigia simu siku hiyo lakini alikataliwa.

"Hapo awali, alikuwa ametuomba tumhamishe kutoka shule hiyo kutokana na adhabu ya viboko lakini nilisisitiza kwamba amalize muhula huu wa tatu. Sikujua ingesababisha kifo chake," mamake mvulana huyo alisema.

Matokeo ya uchunguzi wa maiti yanaonyesha kuwa Kipkoech alikuwa na mishipa iliyoharibika nyuma ya mkono wa kushoto pamoja na uvimbe wa mapafu. Ripoti hiyo pia ilionyesha zaidi kwamba mvulana huyo alikuwa amenyongwa shingo.

"Shule haikunijulisha kifo cha mtoto wangu kama ilivyotarajiwa. Hakuna aliyetuhudumia hata tulipofika shuleni. Tunahisi kwamba shule inafunika kifo cha mtoto wangu. Kuna mtu aliyehusika na lazima akamatwe," alisema baba wa mtoto huyo.

Shule hiyo hata hivyo, imethibitisha kuwa kisa hicho kinachunguzwa na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) katika Kaunti ya Kericho ambapo Afisa Mkuu wa DCI katika Kaunti ya Kericho Rhoda Kanyi amethibitisha kuwa kisa hicho na kusema kuwa bado tukio hilo linachunguzwa na polisi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live