Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi aozeshwa kwa mahari ya nguruwe

Aozeshwa Kisa Nguruwe Mwanafunzi aozeshwa kwa mahari ya nguruwe

Mon, 18 Oct 2021 Chanzo: IPPmedia

Mkazi wa kitongoji cha Mabatini, Wilayani Nkasi mkoani Ruvuma, Kennedy Fumpa (37) amekamatwa kwa tuhuma za kumuoa mwanafunzi wa darasa la tatu kwa kulipa mahari ya shilingi 330,000 pamoja na nguruwe mmoja.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 11 (jina linahifadhiwa), alikuwa darasa la tatu na alilazimika kuacha shule baada ya bibi yake aliyekuwa akimlea kupokea mahari hiyo hivi karibuni na mjukuu wake kuhamia kwa mwanamume huyo ili wakaanze maisha ya ndoa ya mume na mke.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Godfrey Kalungwizi alisema serikali ya kijiji ilipata taarifa kutoka kwa uongozi wa shule kuwa mwanafunzi huyo amekuwa mtoro shuleni kwa muda mrefu ndipo jitihada za kumtafuta zikaanza.

Alisema baada ya jitihada za uongozi wa kijiji kumtafuta mwanafunzi huyo na kumbana bibi aliyekuwa anamlea, alieleza kuwa alikwisha pokea mahari na mjukuu wake huyo tayari amekwisha olewa.

"Baada ya kufuatilia tulibaini kuwa bibi huyo alimuoza mjukuu wake kwa mahari ya Sh. 400,000, ambapo alipokea Sh. 330,000 taslimu na mnyama aina ya nguruwe mwenye thamani ya Sh. 70,000 na kukamilisha kiwango cha mahari alichopangiwa na kumchukua mwanafunzi huyo," alisema.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule aliyokuwa akisoma mwanafunzi huyo, Josephat Joseph, alisema alikuwa haudhurii masomo na kwamba akaorodheshwa katika wanafunzi watoro wa muda mrefu mpaka uongozi wa shule ulipotoa taarifa kwenye serikali ya kijiji na kukamatwa akiwa tayari ameolewa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Peter Lijualikali, alithibitisha tukio hilo na kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo Oktoba 15 na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi na utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Alisema kisichokubalika ni kumbadilisha mtoto wa kike na nguruwe na sheria ya kumlinda mtoto ipo lazima ifuate mkondo wake.

Chanzo: IPPmedia