Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi amcharanga mwalimu wake kwa panga

Panga 3 Mwanafunzi amcharanga mwalimu wake kwa panga

Thu, 28 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sengerema. Mwalimu wa Shule ya Sekondari Tamabu Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Stanford Mgaya, amelazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema akiuguza majeraha yanayodaiwa ni ya kukatwa panga na mmoja wa wanafunzi wake.

Tukio hilo lilitokea juzi, wakati mwalimu huyo, akiwa ofisini akiendelea na majukumu yake ya maandalizi ya masomo ambapo alidai alivamiwa na kuanza kushambuliwa kwa kukatwa panga maeneo mbalimbali ya mwili na mwanafunzi Alex Butawantemi (18), anayesoma kidato cha tatu shuleni hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, alisema tayari mwanafunzi huyo anashikiliwa kwa mahojiano na hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa baada ya kukamilika kwa uchunguzi.

"Ninachoweza kusema kwa sasa ni kuthibitisha tukio hilo na mtuhumiwa tayari anashikiliwa kwa uchunguzi,” alisema kamanda Mutafungwa

Tukio lilivyotokea

Akizungumza na Mwananchi akiwa Hospitali Teule ya Wilaya jana, mwalimu Mgaya alidai mwanafunzi aliyemshambulia ni kati ya wanafunzi 17 wa shule hiyo waliopewa adhabu kwa makosa ya utovu wa nidhamu.

“Kuna wanafunzi walifanya makosa ya utovu wa nidhamu na kupewa adhabu mbalimbali. Wengine walipokea na kutekeleza adhabu zao, lakini huyu mwanafunzi aliyenishambulia aligomea adhabu,” alidai Mwalimu Mgaya.

Alisema akiwa ofisini saa 4:00 asubuhi juzi, Butawantemi aliingia na kumweleza alienda ili wamalizane kuhusu adhabu aliyompa.

“Ghafla alitoa panga alilokuwa amelificha ndani ya shati lake na kuanza kunishambulia… inaonekana alipanga tukio lile,” alidai Mgaya, ambaye hata hivyo alikataa kupigwa picha na mwandishi wa Mwananchi.

Uongozi wa halmashauri

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sengerema, Mwita Waryoba alisema ofisi yake inafanya kila linalowezekana kuhakikisha mwalimu Mgaya anapata matibabu sahihi kusudi apone haraka na kurejea kwenye majukumu yake.

“Jambo la kwanza na muhimu kwetu uongozi wa halmashauri ni kuokoa maisha ya mwalimu Mgaya, ndipo mambo mengine yatafuata,’’ alisema Waryoba.

Kaimu mkurugenzi huyo aliwasihi wazazi na walezi wasiwape tu malezi bora watoto wao, bali pia wafuatilie na kufahamu nyendo zao kuanzia nyumbani na mitaani wanakoshinda.

Naye Mwalimu, Omari Husseni wa Shule ya msingi Tamabu alisema anaamini aliyetekeleza tukio hilo alidhamiria.

"Sidhani kama mwanafunzi huyu alifanya tukio hili kwa bahati mbaya, atakuwa alidhamiria, hivyo ninaomba mamlaka zinazohusika zimpe adhabu stahiki," alisema.

Kwa upande wake ofisa Elimu Shule ya Sekondari, Jenoviva Chuchuba ameomba walimu kutokukatishwa tamaa na tulio hilo, waendelee kuchapa kazi huku vyombo vya dola vikifanya majukumu yake.

Mjomba apigwa butwaa

Pamba John, mjomba wa mwanafunzi Alex aliyemlea baada ya kufiwa na wazazi wake alisema hajawahi kushuhudia wala kupata taarifa za utovu wa nidhamu wa mpwa wake huyo na kushangazwa na kitendo alichokifanya.

“Japo muda mrefu nakuwa mkoani Geita ninakofanya shughuli za kiuchumi, lakini sijawahi kusikia taarifa za utovu wa nidhamu wa huyu mtoto…nataka kwenda hospitalini kumwona na kumjulia hali mwalimu aliyeshambuliwa kwa kukatwa panga na mpwa wangu. Jambo hili siyo tu limenishtua, lakini pia limenivurugia ratiba yangu yote,” alisema Pamba.

Diwani wa Kata ya Tabaruka, iliko shule hiyo, Sospeter Busumabu aliushauri uongozi wa idara ya elimu kuchukua hatua stahiki kukomesha vitendo vya utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live