Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi alipounguzwa kwa pasi siku za kupinga ukatili

6bb8115ddc47c5301e6ec99eb9ff31d3 Mwanafunzi alipounguzwa kwa pasi siku za kupinga ukatili

Tue, 15 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WATU wengi hawawezi kutofautisha kati ya neno jinsi na jinsia. Kimsingi jinsi ni hali ya kuwa mwanamke au mwanaume kwa maana ya maumbile ya kibayolojia, lakini jinsia ni mtazamo wa jamii kuhusu shughuli, majukumu au mtazamo kuhusu makundi ya watu; wanaume, wanawake, watoto, walemavu wazee na kadhalika.

Tunaposema unyanyasaji au usawa wa kijinsia inamaanisha usawa usiojali kundi fulani; wanawake, wanaume, walemavu, wazee, watoto na kadhalika. Aghalabu makundi ambayo yamekuwa yakinyanyasika sana kijinsia na mfumo uliopo ni wanawake na watoto.

Wakati kuna manyanyaso ya kingono yanayowapata watpoto lakini pia kuna manyanyaso ya kudhuru mwili ikiwemo vipigo na kadhalika.

Siku chache zilizopita, dunia likuwa ikiadhimisha siku 16 za kupinga unyanyasaji wa kijinsia ambazo zilikamilika Alhamisi iliyopita.

Lakini wakati siku hizi zikiendelea kuadhimishwa huku kukiwa na matamko kila mahala duniani kote kupinga ukatili wa kijinsia zilishuhudia ukatili wa kutisha wa mtoto wa miaka tisa, anayesoma darasa la pili katika shule ya msingi Chiringe B (jina linahigadhiwa), iliyoko katika halmashauri ya mji wa Bunda, mkoani Mara.

Ukiangalia, madhila aliyopata mtoto ni kwa kuwa tu yeye ni mtoto basi! Mtoto huyo amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kuchomwa na pasi ya umeme na bibi yake kwa madai kuwa alichana shuka yake aliyokuwa amejifunika usiku wa kuamkia siku ya tukio hilo.

Mwenyekiti wa mtaa wa Saranga, Philpo Safari, pamoja na afisa mtendaji wa kata hiyo ya Kabarimu, William Magabo, walithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lililojiri nyumbani kwa mtuhumiwa huyo, Juliana Matutu, maarufu kwa jina Mama Njara.

Akisimluia mkasa huo, Mwenyekiti Safari anasema kuwa baada ya mwanamke huyo kufanya ukatili huo alitokomea kusikojulikana hadi makala haya yanaandikwa alikuwa hajulikani alipo huku mahala alipodai anakwenda baada ya kutejeleza unyama wake ambako ni kwa ndugu zake kulikokuwa na msiba akiwa hajaonekana.

Safari anasema mwanamke huyo alimtelekeza mtoto huyo baada ya kumjeruhi na kumuacha mzee mmoja ambaye ni mkubwa wake hapo nyumbani bila huduma zozote, huku mtoto huyo akiwa anataabika kwa maumivu makali.

“Kwa mujibu ya majirani zake mwanamke huyo baada ya kumaliza kufanya ukatili huo alisema kwamba anakwenda kusalimia msibani, lakini hadi sasa hajulikana alipo,” anasema Safari.

Anayataja maeneo ambayo mtoto huyo aliuunguzwa na pasi kuwa ni kichwani, miguuni, mikononi na sehemu za tumboni.

Anafafanua kuwa tukio hilo lilitokea Jumapili ya Novemba 29, ikiwa ni siku takribani nne tangu kuanza kwa maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia.

Anasema siku iliyofuta mwanafunzi huyo alikwenda shuleni kufanya mtihani wa darasa la pili lakini mwalimu aliyekuwa anasimamia mtihani alimwona mtoto hiyo akitaabika na ndipo akamfuata na kumuuliza kinachomsibu.

Anasema baada ya kuuulizwa mwanafunzi huyo alisema kila kitu alichofanyiwa na bibi yake huku akimwonyesha majeraha hayo.

“Hali ile ilimshangaza sana mwalimu, kuona mtoto anafanya mtihani akiwa na maumivu makali huku akiwa hajapata dawa yoyote,” anasema mwenyekiti huyo wa kijiji.

Afisa mtendaji wa kata ya Kabarimu, William Magabo, anasema kuwa walimu walimchukua mwanafunzi huyo na kumpeleka katika ofisi ya mtaa huo baada ya kumpa huduma ya kwanza.

Anasema kuwa taarifa ilitolewa polisi ikiwa ni pamoja na kumpeleka katika kituo cha afya cha mjini Bunda ambako alitibiwa na kuruhusiwa.

Anasema kuwa kwa sasa mwanafunzi huyo anaishi naye nyumbani kwake kwa usalama wake zaidi, baada ya kukabidhiwa na walimu wake.

Aidha, Mwenyekiti Safari anasema kuwa tayari mkurugenzi wa kituo kimoja cha kulea na kutunza watoto wa aina hiyo kiitwacho Nyumba Salama, kilichoko katika wilaya ya Butiama mkoani Mara, Robhi Samwel, ameshakubalii kumchukua moto huyo ili aweze kulelewa kituoni hapo.

Akisimulia mkasa huo wa kikatili, babu wa mwanafunzi huyo anasema kuwa wamekuwa wakiishi nyumbani hapo na mjukuu wao bila matatizo yoyote na kwamba kitendo alichofanya mtuhumiwa ambaye ni mdogo wake wa tumbo moja ni cha kikatili sana na cha aibu kubwa.

“Tumekuwa tukiishi vizuri hapa nyumbani na huyu mjukuu wetu bila tatizo lolote sasa siku hiyo nilishangaa sana kuona ndugu yangu anafanya kitendo hicho cha aibu, sijui alikuwa na presha gani hiyo,” anasema mzee huyo mwenye umri wa miaka 76.

Akizungumza na gazeti hili mtoto huyo anasema kuwa chanzo cha kufanyiwa ukatili huo ni pale shuka aliyokuwa amejifunika usiku huo ilichanika kwa bahati mbaya kwani imeshazeeka na kwamba ilishakuwa na tundu kubwa katikati kutokana uchakavu.

Baadhi ya majirani akiwemo mjimbe wa shina, Jonathan Bwire, wamelaani kitendo hicho, wakisema kuwa ni cha kinyama na kinatakiwa kukemewa kwa nguvu zote na watu wote.

Chanzo: habarileo.co.tz