Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi achapwa viboko na mwalimu, alazwa hospitali Geita

15020 Mwanafunzi+pic TanzaniaWeb

Sat, 1 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Wakati mtoto Sperius Eradius anayedaiwa kupigwa na mwalimu wake hadi kufariki dunia akizikwa jana wilayani Muleba mkoani Kagera, mwanafunzi wa Sekondari ya Kalangalala mkoani Geita, Jonathan Mkono anadaiwa kupigwa na mwalimu na kulazwa hospitali.

Sperius alifariki dunia Agosti 28, baada ya kupigwa viboko na mwalimu wake kwa madai ya kuiba mkoba wa mwalimu mwingine.

Juzi, mwanafunzi Mkono alipigwa na mwalimu wa nidhamu, Lawson Lechipya kwa kosa la kukutwa bwenini wakati wa vipindi jambo lililomsababishia maumivu makali mwilini.

Kitendo hicho kilisababisha wanafunzi zaidi ya 100 wa kidato cha sita wa shule hiyo kuandamana umbali wa kilomita tatu hadi ofisini kwa mkuu wa Wilaya ya Geita, Josephat Maganga.

Wakizungumza mbele ya Maganga, wanafunzi hao walilalamikia kitendo cha mwenzao kupigwa bakora hadi kulazwa hospitali.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Aron Mathias alisema mwalimu Lechipya alimpiga mwenzao huyo na wengine 10 na kumuumiza zaidi ambapo baadaye alizidiwa na kupelekwa hospitali.

“Baada ya kuzimia tulimpeleka hospitali ya mkoa kwa matibabu na alilazwa wodi namba nane,” alisema.

Akizungumza akiwa katika Hospitalini ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, mwanafunzi aliyepigwa, Jonathan alisema alichapwa bakora hizo na mwalimu wake Agosti 30, saa 12 asubuhi kwa kosa la kuingia bwenini wakati wa vipindi.

“Nilitoka kwenda kusimamia usafi, mimi ni kiranja wa usafi. Baadaye nikaenda bwenini kuchukua vifaa na kukatana na mwalimu wa nidhamu akiwatoa wenzangu na nikajumuishwa,” alisema Jonathan.

Alisema tukio hilo lilitokana na wanafunzi wengi wa kidato cha sita kutoonekana mstarini asubuhi na kwamba, waliamriwa kwenda katika ofisi ya mkuu wa shule na kuanza kuchapwa.

“Alipomaliza kutuadhibu akaja mkuu wa shule na yeye akaanza kutuchapa, wakati mkuu wa shule ananichapa nilianza kujitetea kitendo kilichomkera mwalimu wa nidhamu na kuanza kunichapa tena,” alisema mwanafunzi huyo. “Nililala kifudifudi kujisalimisha, lakini bado aliendelea kunichapa. Kwa mbali niliwasikia walimu wengine wakimwambia ‘acha utamuua’.”

Jonathan alisema baadaye alijikongoja na kuingia darasani kufanya mtihani, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na mchana alirudi bwenini kupumzika.

“Lakini jioni hali ilikuwa mbaya zaidi na wenzangu walinilazimisha na wakanipeleka hospitali na nikalazwa.”

Mwanafunzi huyo alisema hadi sasa bado hawezi kukaa kutokana na maumivu makali anayoyasikia katika maeneo ya kiuno, makalio na miguu yake haina nguvu.

Akizungumzia tukio hilo, mkuu wa wilaya, Maganga aliagiza timu ya wakaguzi kutoka Idara ya Kudhibiti Ubora katika Halmashauri ya Mji wa Geita kufanya uchunguzi na kuandika ripoti atakayoiweka wazi.

“Mdhibiti ubora fanyeni uchunguzi huo kwa umakini mkubwa tayari nimeshatoa maelezo ya awali kwa walimu na ninaamini mtaona mabadiliko makubwa kwenye adhabu zinazotolewa kuanzia sasa,” alisema Maganga.

Mkuu wa shule hiyo, Deusdedt Omuchamba hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo.

Chanzo: mwananchi.co.tz