Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi UDSM auawa na Panya Road Dar

Mwanafunzi Udsm Mauaji Mwanafunzi UDSM auawa na Panya Road Dar

Wed, 14 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Maria Basso (24) amefariki dunia baada ya watu zaidi ya 10 kuvamia nyumbani kwao Kawe Mzimuni.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Septemba 14,2022 na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Wiliam Mkonda imedhibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo Septemba 14 saa 2:30 usiku maeneo ya Kawe mzimuni, kikundi cha wahalifu wakiwa na silaha za jadi, walivamia nyumbani kwa jina Paschal Basso (56).

Amesema baada ya kuvamia nyumba hiyo yenye vyumba 15, walivunja milango na kupora fedha, simu za mkononi, kujeruhi watu watatu na kumuua mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Maria Paschal (24).

"Tukio walilofanya wahalifu hawa ni baya na linalotakiwa kulaaniwa na kukemewa na Mtanzania yoyote anayechukia uhalifu kwa watu kama hawa ambao hawataki kutumia njia halali za kujitafutia kipato," amesema Kamanda Mkonda.

Kufuatia tukio hili, Jeshi la Polisi Kanda Maalum linawasaka wahalifu wote waliohusika katika tukio hilo pamoja na kuimarisha doria za miguu na mgari katika maeneo yote.

“Tunaendelea kuwasisitiza viongozi wa serikali za mitaa na wananchi kwa ujumla kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi katika kukabiliana na uhalifu wa aina hii katika maeneo yao,” amesema.

Shuhuda wa tukio hilo ambaye pia ni jirani Benitto Edward amesema usiku wa kuamkia jana majira ya saa saba usiku, kundi la vijana zaidi ya 20 wakiwa na mapanga, visu, bisibisi na marungu walivamia nyumba hiyo iliyopo Kawe Maringo.

“Baada ya kuvamia nyumba hiyo walianza kuvunja mlango mmoja baada ya mwingine wakiamrisha kupatiwa vitu mbalimbali kama vile simu, fedha na kompyuta mpakato (laptop),” amesema Edward.

Matukio ya watu kuvamiwa yameendelea kushika kasi na kutishia usalama wa wakazi wa jiji la Dar es Salaam ambapo wiki moja tu tangu, Panya Road kuibuka tena na kuvamia nyumba 24 za wapangaji mtaa wa Kabaga Kinyerezi.

Kaimu Amidi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Kamfipo Gidion, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema kuwa Maria alifariki alfajiri ya kuamkia jana kutokana na majeraha aliyoyapata.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live