Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi NIT ahukumiwa miezi 12 jela au kulipa faini Sh5 milioni

73015 Pic+warioba

Mon, 26 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam nchini Tanzania, imemhukumu mwanafunzi wa mwaka wa pili, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Julius Warioba (23) kulipa faini ya Sh5 milioni au kwenda jela mwaka mmoja.

Ni baada ya kukiri shtaka la kuchapisha maudhui katika Mtandao bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Warioba ambaye ni mshereheshaji (MC) anadaiwa kuchapisha maudhui kupitia Televisheni ya mtandaoni ( Tv online) inayojulikana kwa jina Mc Warioba, bila kuwa na kibali kutoka TCRA wakati wakijua kuwa ni kinyume cha sheria ya Mtandao.

Mbali na faini, Mahakama hiyo, imetaifisha kompyuta aina ya Apple na simu ya mkononi aina ya Iphone ambavyo vilitumika katika kuchapisha maudhui hayo.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo amefanikiwa kulipa faini na hivyo kukwepa kifungo.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu Agosti 26, 2019 Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Janeth Mtega baada ya mshtakiwa kutiwa hatiani.

Pia Soma

Hakimu Mtega amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa, hivyo atatakiwa kulipa faini hiyo au kutumikia kifungo.

" Mahakama imekutia hatiani baada ya kukiri kosa lako, hivyo utalipa faini ya Sh5 milioni na ukishindwa kulipa faini hii, utatumikia kifungo cha miezi 12 jela," amesema Hakimu Mtega.

Hakimu Mtega amesema mbali na mshtakiwa huyo kulipa faini, mahakama imeamuru kompyuta na simu moja ya mkononi ya mshtakiwa huyo itaifishwe.

Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon akisaidiana na Batilda Mushi amedai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hilo umekamilika na wako tayari kumsomea mshtakiwa huyo maelezo ya awali.

Simon baada ya kueleza hayo, alimsomea Warioba shtaka lake.

Mc Warioba,  baada ya kusomewa shtaka lake, alikiri na ndipo mahakama hiyo ilipomtia hatiani mshtakiwa huyo na kumhukumu kulipa faini hiyo au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Simon aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali dhidi mshtakiwa huyo, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya kuchapisha maudhui katika Mtandao bila kuwa na leseni kutoka TCRA.

Mc Warioba alifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza, Mei 7, 2019, kujibu shtaka hilo katika kesi ya jinai namba 116/2019.

Katika kesi ya msingi, Warioba anakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha maudhui katika Mtandao bila kuwa na leseni kutoka TCRA.

Tukio hilo anadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Januari 2016 na Aprili 30, 2019 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la  Dar es Salaam.

Inadaiwa katika kipindi hicho,  Warioba alichapisha maudhui kupitia Televisheni ya mtandaoni  (Tv online) inayojulikana kwa jina Mc Warioba, bila kuwa na kibali kutoka TCRA wakati wakijua kuwa ni kinyume cha sheria ya Mtandao.

Chanzo: mwananchi.co.tz