Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi Chuo cha Mipango aburuzwa kortini kwa rushwa

A676f166ee2740f754c78084347cfe0e Mwanafunzi Chuo cha Mipango aburuzwa kortini kwa rushwa

Mon, 1 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoani Dodoma, imemfikisha mahakamani aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) cha Jijini Dodoma, Patrick Abohokile (26) kwa kupokea rushwa.

Amefunguliwa mashtaka manne ya kushawishi Sh 340,000 na kupokea Sh 320,000 kutoka kwa wanafunzi wawili wa mwaka wa tatu wa chuo hicho, waliokuwa wamefanya mtihani wa marudio wa somo la Applied Statistics II ili awasaidie kurudia kufanya mtihani huo nje ya mfumo rasmi wa chuo hicho.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Takukuru mkoani Dodoma, Sosthenes Kibwengo, katika shauri lingine mwanafunzi Rufus Msemwa (32) amefunguliwa mashtaka mawili ya kuahidi na kutoa rushwa Sh 20,000 kwa mwanafunzi mwenzake, ili asaidiwe kurudia mtihani wa somo la Applied Statistics II nje ya mfumo wa rasmi wa chuo hicho.

Kibwengo alisema watuhumiwa hao, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma na kuwafungulia mashauri matatu ya kushawishi, kupokea na kuahidi kutoa rushwa kinyume na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya 2019.

Kibwengo alisema uchunguzi wa Takukuru Dodoma, umefanyika na kubaini kwamba Novemba 2,2020 washtakiwa wakishirikiana na watu wengine ambao bado wanatafutwa, walitenda makosa hayo na kuwezesha baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa tatu wa IRDP kufanya mtihani husika nje ya mfumo, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za chuo.

Mbali na mashauri hayo, Takukuru Dodoma imemfikisha mahakamani Mtendaji wa Kijiji cha Chinugulu wilayani Chamwino, Peter Kyara (36) kwa kosa la kushawishi rushwa ya Sh 500,000.

Uchuguzi wa Takukuru umeonesha Desemba 10 mwaka jana mshtakiwa alimtaka mwananchi mmoja ampatie hongo hiyo, ili asimchukulie hatua baada ya kushtakiwa kwake kwa kosa la kuchunga mifugo kwenye shamba la mwananchi mwingine.

Chanzo: habarileo.co.tz