Dar es Salaam. Mwalimu wa madrasa, Mussa Juma Musa (26) amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kwa tuhuma za ubakaji.
Musa ambaye ni mkazi wa Kinondoni amefikishwa mahakamani hapo jana Jumatano Agosti 21, 2019 kujibu shtaka la kumbaka Leila Moses (22).
Akisomewa hati mashtaka mbele ya hakimu mkazi Caroline Kiliwa, wakili wa serikali Benson Mwaitenda amedai mtuhumiwa alitenda kosa hilo kati ya Oktoba 2018 na Machi 2019 eneo la Mwananyamala.
Mshtakiwa alikana shtaka hilo lakini aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.
Hakimu Kiliwa amemtaka mtuhumiwa kutosafiri bila hati ya mahakama, kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, 2019.
Wakati huohuo, Gabriel Dossa na John Charles walifikishwa mahakamani hapo kwa wizi na uhujumu uchumi wa zaidi ya Sh89 milioni.
Pia Soma
- Kampuni ya Lindi Jumbo ruksa kuchimba madini ya Graphite
- Majeruhi ajali gari la Tanapa wahamishiwa Bugando, Arusha
- Umeme warejea Kagera baada ya kukatika siku tatu
Mbele ya hakimu Frank Mushi, wakili wa Serikali Yussuf Aboud amedai Dossa alitenda kosa hilo Julai 24, 2019 eneo la Kawe (triple 7) wilayani Kinondoni.
Anadaiwa kuiba kebo za Sh47 milioni kinyume na sheria na kuisababishia hasara mamlaka husika.
Charles anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 29 ,2019 maeneo tofauti jijini Dar es Salaam na kusababisha hasara ya Sh42 milioni.
Wakili Aboud amesema watuhumiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kuingilia miundombinu ya kutolea huduma katika jamii.
Kutokana na kutotimiza masharti ya dhamana watuhumiwa walirejeshwa rumande na kesi hiyo kuahirishwa hadi Septemba 4, 2019.