Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu watatu akiwemo Mwalimu wa Shule ya Msingi Mwaselela, Azimio Gerald (31) mkazi wa Mbalizi kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya unyang'anyi wa kutumia silaha, uporaji na uvunjaji wa maduka usiku.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amewataja watuhumiwa wengine kuwa ni Furaha Issa (32) na Goodluck Mwakajisi (25) wote wakazi wa Iwambi, kuwa walikamatwa jana, Alhamisi Januari 25, 2024.
Kuzaga amesema watu hao wanaokabiliwa na tuhuma jihusisha na matukio ya unyang'anyi wa kutumia silaha, uporaji, uvunjaji wa nyumba, maduka na wizi, walikamatwa na askari waliokuwa doria.
Amesema baada ya kupekuliwa wamekutwa na vitu vya wizi ikiwemo televisheni mbili, redio subwoofer tatu, redio ndogo nne na spika zake, laptop nane, simu za mkononi 16 na mashine moja ya kupimia damu.
Aliongeza kuwa, watuhumiwa walikutwa na vifaa mbalimbali vya kuvunjia nyumba na maduka, visu vinne, mapanga matatu na baadhi ya mali zimetambuliwa na walioibiwa.
“Nitoe wito kwa wahalifu wote watambue kuwa Jeshi la Polisi halijalala litaendelea na misako ya kupambana na uhalifu kwa kushirikiana na polisi jamii na ulinzi shirikishi,” amesema.
Pia ameonya tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali za mitaa kuacha tabia za kushirikiana na wananchi kujichukulia sheria mikononi kwa wahalifu na kwamba wakibainika sheria itachukua mkondo wake.
Mkazi wa Forest jijini hapa, Salome Joel ameomba Jeshi la Polisi kutoa elimu wa viongozi wa Serikali za mitaa kutekeleza majukumu yao na kuepukana na chuki, fitina na kuwabambikiza watu kesi.