Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwalimu mbaroni kwa kubaka mwanafunzi

15482 Mwalimu+pic TanzaniaWeb

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kiteto. Mwalimu wa shule ya sekondari Engusero wilayani Kiteto mkoani Manyara, Henry Michael (30) amefikishwa mahakamani na kusomewa shtaka la kumbaka kichakani msichana wa kidato cha pili wa shule hiyo. 

Mwendesha mashtaka wa kesi hiyo, mkaguzi wa polisi, Mbaruku Makame akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kiteto, Majid Hudi alisema Michael anadaiwa kutenda tukio hilo Agosti 26, 2018 saa 2 usiku eneo la shule hiyo. 

Makame alisema mwalimu huyo alimbaka mwanafunzi huyo baada ya kumtuma nyumbani kwake akamletee vifaa vya kufundishia shuleni. 

Alisema mwanafunzi huyo anaishi na wenzake kwenye bweni la shule hiyo ndipo usiku huo akamuita na kumuagiza aende nyumbani kwake naye akamfuata kwa nyuma na kumshika kwa nguvu kisha akambakia kichakani. 

Alisema baada ya kufanyiwa tukio hilo, mwanafunzi huyo alitoa taarifa kwa uongozi wa shule hiyo ambao walifikisha suala hilo kituo kidogo cha polisi Matui na mtuhumiwa kukamatwa na kufikishwa kituo cha polisi Kibaya. 

Alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 130 (1) (2) (e) na 131 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo mwalimu Michael alikana shtaka hilo mahakamani hapo alipoulizwa na Hakimu Hudi kama ni kweli alitenda kosa hilo. 

Hakimu Hudi aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 7, 2018 itakapotajwa tena mahakamani hapo kwani upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. 

Mashtakiwa Michael alipelekwa mahabusu kwenye gereza la wilaya mara baada ya kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wenye Sh2 milioni kila mmoja. 

Watu wengi walijitokeza kwenye mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo baada ya kupata taarifa kuwa mwalimu Michael anashikiliwa kwenye kituo cha polisi Kibaya. 

Chanzo: mwananchi.co.tz