Mahakama ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara imemhukumu kifungo cha kwenda jela maisha Idrisa Athuman Naleja aliyekuwa mwalimu katika Shule ya Msingi KYAWAZARU iliyopo wilayani Butiama mkoani humo kwa kosa la kumlawiti mwanafunzi.
Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali, Gaston Kayombo mbele ya Hakimu mkazi Mwandamizi Khadija Msala, Idrisa Naleja alitenda kosa hilo mwezi Aprili mwaka 2022 kwa nyakati tofauti ambapo mara ya kwanza ilikuwa katika shamba lililopo karibu na Shule ya Kywazaru na mara ya pili ni ofisi kwake baada kuondoka kwa walimu na wanafunzi.
Katika kesi hiyo ya Jinai namba 54 ya mwaka 2022, Jamhuri ilikuwa na mashahidi sita akiwemo mwathirika wa tukio hilo na daktari aliyethibisha tukio hilo kutendwa baada ya vipimo mbalimbali vya kitabibu.
Hakimu mkazi Mwandamizi akitoa hukumu hiyo amesema mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume na Kifungu cha 154, kifungo kidogo cha 1(a) na cha pili cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya Mwaka 2022.
Hukumu ya kesi hiyo ni moja ya hukumu kati ya kesi nane zilizokuwa zikimkabili Idrisa Athuman Naleja ambazo saba bado hazijatolewa uamuzi na hii ni baada ya kufanya vitendo vya ulawiti kwa wanafunzi wanane.