Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwalimu apoteza maisha kwa kushambuliwa

Mauaji Katembo Kamanda Mwalimu apoteza maisha kwa kushambuliwa

Sat, 13 Aug 2022 Chanzo: ippmedia

Mwalimu wa Shule ya Mwingi Mbaju, Masasi mkoani Mtwara, Mwanahawa Shaibu (50) ameuawa kwa kushambuliwa Hadi kufa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi (ACP) Nicodemus Katembo, alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo huku akisema limetokea juzi majira ya saa 1:00 usiku katika kijiji cha Mbemba kata ya Chigugu.

Alisema, mwalimu huyo kabla ya kukutwa na umauti, alikuwa akitokea shuleni kwenda  nyumbani Mbemba.

Kamanda Katembo alisema wakati akirudi nyumbani akiwa amepakiwa kwenye pikipiki, alimkuta mtu akiwa amelala barabarani na aliposimama ili kujua mtu huyo amekutwa na matatizo gani hadi kufanya hivyo, ndipo aliposhambuliwa ghafla na mtu huyo.

Katembo alisema, mwalimu huyo alipojaribu kutoa msaada kwa mtu huyo ambaye walikumkuta amelala barabarani, mtu huyo alianza kumshambulia mwalimu  bila  sababu yoyote.

Alisema, mwalimu huyo baada ya kushambuliwa kwa kutumia mawe kumpiga, alianguka na kupoteza maisha.  Kutokana na mauaji hayo, alisema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi.

Kamanda Katembo alisema tayari mwili wa marehemu umeshakabidhiwa kwa ndugu na jamaa kwa ajili ya mazishi.

Katika hatua nyingine, katembo alisema kwa sasa wilaya ya Masasi imekuwa na matukio ya mauaji hasa kwa wanawake na kwamba tangu Machi, mwaka huu,  matukio nane ya mauaji yameshatokea hadi sasa.

Alisema, kutokana na matukio hayo, Jeshi la Polisi litahakikisha wahusika wote wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo ya sheria.

Chanzo: ippmedia