Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwalimu ‘aliyeoa’ mwanafunzi na kukamatwa, adakwa tena akiishi naye

29196 Pic+mwalimu TanzaniaWeb

Wed, 28 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Buchosa. Endapo itathibitika pasipo shaka kwamba Mwalimu Michael Ikila ameishi tena kinyumba na mwanafunzi yuleyule aliyewahi kuelezwa kukutwa akiishi naye, basi usemi wa “Sikio la kufa halisikii dawa” utasadifu kwake.

Mwalimu huyo wa Shule ya Sekondari Nyakasungwa, Buchosa wilayani Sengerema alikamatwa Septemba 21 akituhumiwa kuendelea kuishi kinyumba na mwanafunzi wake akiwa bado yuko chini ya uchunguzi kwa kosa hilo. Mwanafunzi huyo alihitimu kidato cha nne mwaka 2016 na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Mkinga, Tanga mwaka 2017 lakini hakuripoti baada ya kuanza kuishi kinyumba na mwalimu hiyo. Baada ya kukamatwa kwa kosa hilo, Mwalimu Ikila alitakiwa kuripoti polisi kwa uchunguzi zaidi.

Wakati uchunguzi dhidi yake ukiendelea na kutakiwa kuripoti polisi, ilielezwa kuwa Mwalimu Ikila na mwanafunzi huyo waliamua kuondoka Sengerema na kuhamishia makazi yao Mtaa wa Nyamazobe, Mwanza na kukamatwa juzi.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alisema taratibu za kumfikisha mahakamani mwalimu huyo zinaendelea.

“Lazima aadhibiwe kwa mujibu wa sheria kwa sababu kitendo chake sio tu kinakiuka maadili na miiko ya ualimu, bali pia ni uvunjifu wa sheria,” alisema Kipole.

Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Buchosa ya Wilaya, John Busiga alisema pamoja na mtuhumiwa kufikishwa mahakamani, mwanafunzi huyo atarejeshwa shuleni na atalazimika kukariri kidato cha tano.

Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Michael Ligola aliyefanikisha mtuhumiwa kutiwa mbaroni alisema tayari ofisi yake kwa kushirikiana na vyombo vingine imeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma za baadhi ya walimu wilayani Sengerema kudaiwa kujihusisha kingono na wanafunzi wao.

Mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Maria Kimbambeze aliyezungumza kwa simu juzi, alisema mtoto wake alianza kuishi kinyumba na mwalimu huyo baada ya kutoroshwa mara tu alipomaliza mitihani ya kidato cha nne mwaka 2016.

“Baada ya kumaliza mitihani na matokeo kutoka kuwa anatakiwa kuendelea na kidato cha sita, familia ilishindwa kumudu kumlipia gharama; kitendo hicho kilimfanya mtoto kubaki nyumbani kabla ya kutoshwa na mwalimu wake kwenda kuishi naye kama mume na mke,” alisema.

Alisema alishindwa kumlipa gharama za masomo binti yake baada ya mumewe kufariki dunia.



Chanzo: mwananchi.co.tz