Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwalimu adaiwa kujinyonga

Kifo Kifo Mauiaji.png Mwalimu adaiwa kujinyonga

Tue, 5 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mratibu Elimu Kata Angelus Mwinyuku (46) ambaye ni mkazi wa Jida wilayani Masasi, mkoani Mtwara, adaiwa kujinyonga katika ofisi za Chama cha Walimu (CWT), huku Jeshi la Polisi mkoani hapa likisema linafanya uchunguzi wa tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 05, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nikodemus Katembo amesema kuwa tukio hilo lilitokea saa 12 jioni katika ofisi za CWT zilizopo katika Mtaa wa Wapiwapi, wilayani Masasi.

Kwa mujibu wa Kamanda Katembo, marehemu alikuwa Mratibu wa elimu katika Kata ya Matawale na alikutwa bafuni akiwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya manila, iliyokuwa imefungwa kwenye dirisha la bafu hilo katika ofisi hizo za CWT.

Katembo amesema kuwa baada ya Polisi kupokea taarifa ya tukio hilo, askari wake walifika eneo hilo kwa uchunguzi zaidi.

Hata hivyo, jeshi hilo limesema katika uchuguzi wa mwili uliofanywa na daktari ulibaini kuwa chanzo cha kifo hicho ni kukosa hewa baada ya kujifunga kamba shingoni, huku sababu za kufanya hivyo zikiwa bado hazijafahamika.

“Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi kuwa makini na kuendelea kuchukua hatua na tahadhari ili kuepuka vitendo vya kujinyonga.

“Vema kushirikisha watu wa karibu pale wanapopata changamoto za kimaisha,” ameasa mkuu huyo wa Polisi mkoani Mtwara.

Watumishi wenzake

Mratibu Elimu, Kata ya Chanikanguo, Methew Andelile akiwa msibani hapo amesema kuwa wapo waratibu elimu kata 14 waliofanya kazi kwa ukaribu na marehemu ambapo wamesikitishwa na tukio hilo.

“Tupo waratibu elimu kata 14 tumefanya kazi kwa ukaribu, alionyesha ushirikiano mkubwa, mara kadhaa tumekuwa pamoja kwenye vikao na semina tunasikitika kumpoteza ni pengo kubwa kwa tasnia ya elimu Masasi Mji, apumzike kwa amani,” amesema Andelile.

Kwa upande wake Daniel Masebo, ambaye ni Mratibu Elimu Kata Migongo, amesema anashindwa kuelewa jambo lililomsibu marehemu.

“Tukio lenyewe limetushtua hatuelewi ilikuwaje na kwa nini limetokea, ila mara ya mwisho ni wiki iliyopita tulikuwa naye kwenye semina ambapo alisema anatumia dozi ya Malaria na akasema anajisikia vibaya akaondoka tangia hapo hatujaonana naye,” Masebo.

Mwenyekiti wa Maofisa Elimu Kata katika Halmashauri ya Mji Masasi, Hamis Chakulya amesema kuwa licha ya kuwa marehemu alikuwa mfanyakazi mwenziye, lakini alikuwa ni rafiki pia, kifo chake kimeacha pengo kubwa kwake.

“Tulifanya kazi kwa ukaribu, alikuwa rafiki yangu ambaye tulikuwa tunabadilishana mawazo hata safari nyingi tulisafiri pamoja alikuwa mcheshi sana, muongeaji mzuri ni mtu ambaye alikuwa wa karibu na kila mtu,” amesema Chakulya na kuongeza;

“Hakuwa mchoyo hata ukikwama kipesa hakuwa mchoyo, hata gari yake ukiwa na safari ukimuomba anakupatia, mara mwisho nikiwa mafunzoni niliangalia kwenye semina sikumuona nikalazimika kumpigia...akasema hajisikii vizuri anaumwa nikamsihi aje na alikuja na akashiriki lakini hakumaliza alisema hawezi kuendelea kwa kuwa anajisikia vibaya akaondoka,”amesema Chakulya.

kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Lauther Kanoni amesema kuwa mwalimu huyo alikuwa ni mweka hazina wa CWT, Wilaya ya Masasi.

"Siku ya tukio wanasema kuwa asubuhi aliKWenda kanisani kwenye ibada ya Jumapili aliporudi akaenda kwenye ofisi za CWT Wilaya ya Masasi, kwa kuwa alikuwa Mweka hazina hakuna aliyemtilia shaka wakajua anaenda kufanya kazi zake kumbe alikuwa akienda kutekeleza tukio hilo,” amesema Kanoni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live