Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwaipaya kufikishwa mahakamani

TWAHA DODOMA POLISI Mwaipaya kufikishwa mahakamani

Sun, 10 Jul 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Polisi Mkoani Dodoma wanatarajia kumfikisha Mahakamani Mratibu wa uhamasishaji wa Baraza la vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Twaha Mwaipaya.

Mbali na Mwaipaya, Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Martin Otieno alisema Jeshi hilo pia linawashikilia watu wawili kwa makosa ya kimtandao, akiwamo Frank Trifoni anayedaiwa kujifanya kuwa ni Waziri wa Ardhi, Angelina Mabula na kufanya vitendo vya kitapeli.

Mwingine ni Charles Masanja anayeshikiliwa kwa kosa la kujifanya mtumishi wa Tamisemi kisha kuwadanganya watu kuwa atawapa ajira kwenye kazi ya sensa inayokwenda kufanyika nchini mwaka 2022.

Kamanda huyo alisema Mwaipaya atafikishwa mahakamani hivi karibuni baada ya uchunguzi wa kosa lake la uhalifu wa kimtandao utakapokamilika.

Mwaipaya alikamatwa Juni 30 mkoani Morogoro na kupelekwa Dodoma siku kadhaa, alisota mahabusu ya polisi pasi kupatiwa dhamana wala kufikishwa Mahakamani.

Kitendo hicho, kilikisukuma Chadema kuamua kufungua kesi ya maombi madogo ya jinai 25/2022 katika Mahakama Kuu Kanda ya Kati dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kamanda wa Polisi na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya (OCD) Dodoma, wakishinikiza kuachiwa kwa mfuasi huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda Otieno alisema Mwaipaya anakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya mtandao ambapo anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo kupitia ukurasa wake wa Twiter kuhusu bei za umeme.

Alidai kuwa Otieno alitenda kosa hilo kinyume na sheria kwa sababu yeye si msemaji wa Shirika la umeme au msemaji wa Serikali, hivyo alisababisha kuzua taharuki kwa wananchi.

“Mwaipaya, tunaendelea na uchunguzi na muda wowote tutamfikisha Mahakamani, yeye si msemaji wa Serikali, alitumia utaratibu alioona unafaa na kuzua taharuki kuwa Serikali imepandisha bei za umeme,”alidai Kamanda Otieno.

Akimzungumzia Frank Trifon na Charles Masanja, Kamanda Otieno alidai wamekuwa na rekodi ya kutapeli watu kwa njia ya mtandao kwa kujifanya maofisa na mmoja Waziri wa Ardhi, hivyo walikuwa wakifuatiliwa.

Polisi pia imewakamata watu 42 wanaodaiwa pia kujihusisha na uhalifu wa kuvunja, matumizi ya bangi na wizi wa pikipiki.

Alisema kupitia oparesheni iliyofanywa na kikosi maalumu cha jeshi hilo, wamefanikiwa kuwakamata watu hao wakiwa na pikipiki 25, kompyuta saba, visimbuzi vitatu, shaba tatu, mbegu za bangi na milango 22 na mbao zilizovunwa kinyume cha sheria.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz