Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvuvi kizimbani akidaiwa kuua watu watano

Mon, 11 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Yusuph Said (40), mvuvi mkazi wa Mbagala Zansa jijini Dar es Salaam amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Ijumaa Februari 8, 2019 akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya bila kukusudia ya watu watano.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya hakimu mkazi mwandamizi, Janeth Mgeta wakili wa Serikali, Esta Martine amedai Mei 27, 2016 katika ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Kigamboni, mtuhumiwa anadaiwa kumuua, Shangai Dimbwa bila kukusudia.

Martine amedai siku hiyo mahali pa tukio la kwanza, mshtakiwa aliwaua bila kukusudia Feisal Khamis, Thomas Nyoni, Erick Kilunga na Masuke Maduhu.

Martin amedai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya kusomewa shtaka la mauaji bila kukusudia kesi namba PI07/2019 mshtakiwa alikana mashtaka yote.

Hakimu Mgeta alimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua zinazotoka kwa mkurugenzi wa manispaa husika, kuwa na kitambulisho cha Taifa au cha kupiga kura  watakaosaini  bondi ya Sh4 milioni kila mmoja.

Pia alimtaka mshtakiwa  kuwasilisha hati yake ya kusafiria mahakamani, asitoke nje ya nchi na kuripoti kituo cha polisi cha wilaya karibu na makazi yake.

Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurejeshwa rumande hadi Februari 21, 2019 itakapotajwa tena.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz