Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvutano waibuka kortini kesi ya kina Ole Sabaya

SABAYAAA ED Mvutano waibuka kortini kesi ya kina Ole Sabaya

Sat, 21 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, imeahirisha kuendelea kusikiliza kesi ya jinai inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake baada ya mawakili wa utetezi kupinga uhalali wa wakili wa Jamhuri kumhoji shahidi wa pili wa utetezi Silvester Nyegu (26) .

Akihojiwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, shahidi huyo wa utetezi alidai mahakamani huko kwamba hakuwahi kuandika maelezo yoyote kituo cha polisi, wala kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Vilevile, shahidi huyo alidai kwamba anafahamu kuwa endapo mahakama hiyo itamtia hatiani kifungo chake kitakuwa cha maisha au miaka 30.

Wakili Kweka aliiomba mahakama hiyo kutumia kifungu namba 154 cha Sheria ya Ushahidi kutumia maelekezo ya shahidi aliyoandika kituo cha polisi kumhoji.

Wakili huyo alidai kwamba kwa mujibu wa utaratibu wa kisheria, maelezo hayo yanaweza kuwa ya shahidi au kumhusu mwenyewe, pia sio lazima maelezo yawe yameandikwa na shahidi na wakati mwingine sio lazima aonyeshwe maelezo hayo mahakamani kwa kuwa ni matakwa ya kisheria.

"Tunachokifanya hapa kimekidhi kigezo cha kifungu cha Sheria ya Ushahidi Na. 154, na katika muktadha huo kwa kuokoa muda wa mahakama, tunaomba ombi la utetezi litupiliwe mbali na turuhusiwe kuendelea kumhoji shahidi huyu," alidai Wakili Kweka.

Wakili wa Utetezi, Edmund Ngemela, alipinga vikali maelezo hayo yanayodaiwa ni ya shahidi huyo kutumika kumhoji kwa kuwa sheria imeelekeza, ili kumuuliza maswali shahidi, maelezo yanatakiwa kuwa yameandikwa na muhusika mwenyewe.

“Shahidi ameieleza mahakama kwamba maelezo hayo hayafahamu na hakuwahi kuhojiwa popote, hivyo tunaomba mahakama kukataa jambo hilo na kielelezo chenyewe siyo kwa sababu hakijapokelewa mahakamani na hauwezi kumhoji shahidi wakati kielelezo hicho hakijapokelewa kisheria,” alidai.

Wakili mwingine wa Utetezi, Silvester Kahunduka, alidai mahakamani huko kuwa  kifungu cha sheria ya ushahidi namba 154 kilichotumiwa na wakili wa serikali hakikufuata takwa la kisheria.

“Wakili anasema shahidi aliwahi kuandika maelezo polisi wakati shahidi anadai kwamba, hakuwahi kuandika maelezo sehemu yoyote na tunatumaini kwamba mteja wetu hatatendewa haki, maelezo hayo yasitumike kumhoji maswali kwa kuwa hayafahamu," alidai.

Baada ya mvutano huo wa kisheria, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Odira Amworo, aliahirisha kesi kwa dakika 15 kwenda kupitia hoja za mawakili hao.

Hakimu Mwandamizi wa Mahakama hiyo, alidai mahakamani huko, kwamba baada ya kupitia hoja hiyo na kufanya uchunguzi wake hakufikia mwisho kwa kuwa jambo hilo halikuwa dogo kama mawakili hao walivyodhani.

“Katika kupekua na kupitia hoja zenu, nimeona kuna maswali mengi yamejitokeza hivyo tunaahirisha kusikiliza shauri hili hadi Agosti 23 mwaka huu, nitatoa uamuzi mdogo kwa kuwa pande zote zipo kwa ajili ya kutafuta haki,”alisema Hakimu Odira.

Mbali na Sabaya na Nyegu, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Daniel Mbura (38).

Chanzo: ippmedia.com