Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muuguzi auawa baada ya kutuhumiwa kuua

53727 Pic+muuguzi

Tue, 23 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora. Muuguzi katika hospitali ya wilaya ya Urambo, Oscar Mwakipesile ameuawa baada ya kupigwa na kundi la watu kutokana na tuhuma za kumuua mkazi wa kijiji cha Izimbili wakati wakicheza muziki.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley amesema tukio hilo limetokea jana Jumatatu ya Pasaka saa saba usiku.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Nley amesema muuguzi huyo anadaiwa kumtuhumu Masoud Joackim kumshika shika mkewe sehemu mbalimbali za mwili wake yakiwemo makalio.

Amesema muuguzi huyo alikasirika na kumchoma na kitu chenye ncha kali kifuani Masoud upande wa kushoto na kufariki.

Amesema watu waliokuwa wakicheza muziki, walimfukuza na kumkamata baada ya umbali wa mita 500 na kumpiga kwa mawe mwilini na kichwani hadi kumuua.

Amedai kuwa marehemu wote wawili walikuwa wamelewa pombe na kuwa Polisi inawashikilia watu wawili kuhusiana na tukio hilo na kuwataja watu hao kuwa ni John Mashaka na David Ngumie na upelelezi zaidi wa tukio hilo unaendelea.

Adam Malunkwi ambaye ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Urambo ambaye pia ni diwani wa kata ya Uyumbu lilipotokea tukio hilo amesema marehemu Mwakipesile aliwahi kufanya kazi zahanati ya Izimbili na alikuwa amewekeza katika biashara ya kupiga muziki au disco.

Kwa upande wa Amatus Ilumba ambaye ni diwani wa kata ya Urambo ilipo hospitali ya wilaya alipokuwa akifanya kazi muuguzi huyo, amesema wamepokea kwa masikitiko msiba huo na kwamba walikuwa katika pilikapilika za kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Mbeya.

Alipopigiwa mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Urambo, Dk Ismail Kanani, simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa.



Chanzo: mwananchi.co.tz