Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muuguzi anaswa na begi la dawa za serikali

01e848d374ea632906953759927fb8f0 Muuguzi anaswa na begi la dawa za serikali

Mon, 21 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Katavi, inafanya uchunguzi wa wauguzi watatu wa Kituo Cha Afya Ilembo kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, kwa tuhuma za wizi wa dawa za serikali na kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wagonjwa waliokuwa wamelazwa kwenye kituo hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi, Christopher Nakua alisema Hussein Hassan ni mmoja wa wauguzi hao, ambaye alikamatwa na begi likiwa na dawa za binadamu, ambazo ilibainika alikuwa akiwauzia wagonjwa kwenye wodi ya wazazi hasa nyakati za usiku.

"Hussein muuguzi kwenye wodi ya wazazi alikamatwa Desemba 14,2020, baada ya kuanza kuhojiwa na uongozi wa kituo hicho na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda alikiri kutenda kosa hilo lakini alikimbia kwa lengo la kujaribu kutoroka na aliacha pikipiki yake,"alisema Nakua.

Alisema muuguzi Charles Daniel aliye kwenye wodi ya wazazi katika kituo hicho, alibainika kuomba rushwa kwa mume wa mgonjwa aliyekuwa amelazwa katika kituo hicho.

"Desemba 13, 2020 majira ya saa 2:00 usiku aliomba rushwa ya shilingi 20,000 lakini alipewa shilingi 10,000 na mume wa mgonjwa huyo ili amsaidie mgonjwa wake kujifungua salama,"alisema.

Alisema uchunguzi wa awali umeonesha baada ya muuguzi huyo kubanwa na Muuguzi Mfawidhi na Kaimu Mganga Mkuu wa kituo hicho, alirudisha Sh 10,000 kwa mhusika.

Alisema muuguzi wa tatu, Isack Muhigi Desemba 13, 2020 mchana alimuomba mgonjwa rushwa ya Sh 10,000 na kupokea fedha hiyo ili amsaidie mgonjwa kupatiwa huduma ya kujifungua salama.

Baada ya kubanwa, pia alimrudishia mgonjwa huyo pesa yake mbele ya Kaimu Mganga Mkuu wa kituo hicho.

Takukuru Mkoa wa Katavi inaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo pindi utakapokamilika na kuthibitika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Chanzo: habarileo.co.tz