Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mume wa Shamimu akana vielelezo mahakamani

Abdul Nsembo.jpeg Mume wa Shamimu akana vielelezo mahakamani

Thu, 1 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MFANYABIASHARA Abdul Nsembo anayekabiliwa na kesi ya kusafi risha dawa za kulevya, amekataa kuvitambua vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani na fomu ya ukamataji wa vielelezo hivyo, inayodaiwa kuwa aliisaini nyumbani kwake baada ya upekuzi usiku wa kuamkia Mei 1, mwaka jana.

Katika kesi hiyo kwenye Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa, Nsembo alivikana vielelezo hivyo jana mbele ya Jaji Elinaza Luvanda.

Mshitakiwa huyo alisisitiza ombi lake kwamba Mahakama iruhusu picha za kamera za CCTV ya nyumbani kwake zilizorekodiwa siku hiyo, ziwasilishwe mahakamani ili kuthibitisha madai yake.

Akiongozwa na Wakili wake, Juma Nassoro Nsembo alidai kuwa baadhi ya vikopo katika vielelezo namba 3 B mpaka E, hakuwahi kuviona kabla na pia vile ambavyo aliwahi kuviona wakati wa kufunga vielelezo ka- tika Tume ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya, vyote vilikuwa na unga wa njano, badala ya ule wa kaki, aliouona mahakamani jana.

“Vielelezo namba B na D sikuwahi kuviona na hata hivyo vingine vilikuwa na unga wa njano vyote, ambao ulikuwa katika vikopo vidogo na havikuwa vimejaa, vilikuwa na ujazo wa nusu wa vikopo, tofauti na hivi ninavyoviona hapa vimejaa,”alidai Nsembo.

Alidai kuwa hati ya ukamataji, hakuisaini nyumbani kwake, bali aliisaini Mei 13 akiwa kituo Kikuu cha Polisi na haikuwa imekamilika, kama ile iliyowasilishwa mahakamani.

“Mimi nililetewa fomu tu ya uthibitisho kwamba tulifanyiwa upekuzi ambayo ilikuwa na majina mawili, langu na Shamim mke wangu.

Hakukuwa na majina mengine yoyote, tofauti na hii ninayoiona hapa ina majina mengine ya mashahidi na hati yenye orodha ya vielelezo vilivyokamatwa ambayo sikuwahi kuiona hapo mwanzo.

Hii karatasi yenye orodha ya vielelezo, sikuwahi kuiona mahali popote zaidi ya hapa leo” alisema.

Nsembo pia alikana kumfahamu shahidi wa 7 wa upande wa Jamhuri, Nassoro Athumani ambaye alijitambulisha kuwa ni mlinzi wa ulinzi shirikishi katika Mtaa wa Upendo, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam anakoishi Nsembo.

“Jambo muhimu ambalo naomba Mahakama yako ifahamu ni kuwa shahidi namba 7, Nassoro Athumani aliyejitambulisha kama mlinzi shirikishi siyo wa kweli, kwa sababu mtaa ninaoishi kila mmoja ana ulinzi wake, hakuna ulinzi shirikishi.

Mimi naishi pale miaka mingi na ninashiriki vikao vya maendeleo, simfahamu kabisa Nassoro na sijawahi kulipa ada ya ulinzi shirikishi, hiyo inamaanisha hakuna ulinzi shirikishi kwenye mtaa wetu,” alisema.

Nsembo alidai kuwa kesi hiyo imetengenezwa, kwa kile alichodai kuwa ni ugomvi baina yake na Inspekta Msaidizi wa Polisi, Salmin Sherimo ambaye ndiye alikuwa msimamizi wa kazi ya upekuzi siku hiyo, kwa madai kuwa waliwahi kukwaruzana mwaka 2014.

“Hii kesi ilianzia kwenye ugomvi wangu na Salmin ambaye alinikamata mwaka 2014 wakati wa ukaguzi wa magari yaliyotoka Afrika Kusini.

Alikamata gari langu Mercedes Benz na mimi, alinipeleka kituo kikuu cha Polisi akitaka niwasilishe nyaraka halali za gari hilo, kulitokea kutoelewana tukafikia kujibizana vibaya lakini baadaye nilishinda na kurudishiwa gari, na yeye hakuridhika akaahidi kuwa atanikomesha na ni yeye huyo aliyeongoza askari kupekua nyumbani kwangu hiyo Mei 1,” alidai Nsembo.

Awali akiongozwa na Wakili wa Utetezi, Juma Nassoro Nsembo alieleza namna askari walivyokwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake Mei 1, 2019.

Alisema kuwa siku hiyo alikuwa nyumbani kwake na familia yake; na askari walimkuta chumbani kwake akiwaangalia kwenye CCTV, tofauti na ilivyodaiwa awali kwamba alikutwa juu ya dari.

“Ilikuwa ni majira ya usiku tulikuwa tumelala na familia yangu, nikasikia kelele nje za geti likigongwa, nilitazama kwenye CCTV nikaona kundi la watu wapatao ishirini wakiwa nje ya geti huku wengine wakiwa wamepanda juu ya geti.

Nilihisi nimevamiwa na majambazi, nikamchukua mke wangu na watoto nikawaambia waende chumbani kwa dada wa kazi na mimi nikabaki chumbani nikiangalia picha za CCTV”alisema.

“Walikuwa wakiongea na kijana wangu wa kazi, ambaye nilimuona baadaye akizunguka nyuma ya nyumba na kugonga dirisha la chumba cha dada ambako na mke wangu alikuwemo, baada ya muda mfupi mke wangu alikuja na kuniambia walikuwa ni askari wanamwita nikamruhusu aende,”alisema Nsembo.

Alidai kuwa baada ya mke wake kutoka, alimuona akiwafungulia mlango na wakaingia ndani ya uzio.

Mkewe aliingia ndani na hakujua alienda kufanya nini, lakini alipotoka alimuona akitoa ishara kidole kuelekea mlango wa gereji ya kulaza magari na kijana wake wa kazi akafungua milango hiyo, iliyokuwa imeegeshwa.

Nsembo aliendelea kudai kuwa baada ya kuingia gereji, hakujua nini kiliendelea, kwa kuwa kamera ya CCTV haikuwa katika eneo hilo, lakini aliwaona wakitoka baada ya muda wakiwa hawana chochote.

Alisema, waliendelea kupekua ikiwa ni pamoja na kwenye magari yaliyokuwa ndani ya uzio, vyumbani, jikoni na baadaye wakaingia chumbani kwake, ambako walimkuta na kumfunga pingu kisha walianza kupekua chumba hicho na baadaye wakawatoa nje ya uzio wa nyumba.

Nsembo alidai hapo nje, waliendelea kukaa wakiwa na askari watatu wa kiume na mmoja wa kike; na wengine walibaki ndani kwa muda usiopungua dakika 20 na hawakujua nini kinaendelea ndani.

Awali, Nsembo aliomba Mahakama iruhusu picha za CCTV ziwasilishwe mahakamani, kama sehemu ya ushahidi wake. Mahakama iliruhusu, lakini picha za CCTV zilishindwa kutumika, kwa sababu password alizotoa zilikataa kufungua ‘server’ ya kamera hizo, lakini yeye alisisitiza kuwa ndiyo halisi.

Kesi hiyo itaendelea kesho ijumaa.

Chanzo: habarileo.co.tz