Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mume amuunguza mkewe, mwanaye ‘kwa petroli’

65420 PIC+MOTO

Thu, 4 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Elias Warioba,  anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kwa tuhuma za kumjeruhi mkewe, Mkami Mbarahi (19) na mwanaye wa miezi mitatu baada ya kuwarushia chupa iliyokuwa na mafuta ya petroli na kusababisha walipukiwe na moto na kupata majeraha maeneo mbalimbali mwilini.

Mwanamke huyo aliyerushiwa chupa hiyo akiwa jikoni anapika, ni mkazi wa kijiji cha Mlazo kata ya Ng’hambako tarafa ya Mpwayungu Wilaya ya Chamwino, amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma pamoja na mwanaye.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Julai 3, 2019 Mkami amesema siku ya tukio Juni 28, 2019 akiwa anaandaa chakula usiku huku akiwa amembeba mwanaye mgongoni, mumewe alifika nyumbani akiwa na chupa hiyo kwa ajili ya kujaza mafuta katika pikipiki.

Amesema mumewe alihoji sababu za kutumia kuni kupika akidai anaweza kuunguza kibanda, alipomjibu kuwa hawezi kuunguza kibanda hicho, alimrushia chupa hiyo iliyompiga kichwani na kumwagikiwa na mafuta.

“Mfuniko wa ile chupa ulifunguka na mafuta yalinimwagikia na moto kutulipukia. Nilianza kupiga kelele kuomba msaada wa majirani lakini mume wangu hakujali aliondoka bila kutoa msaada,” amesema Mkami aliyeungua kichwani hadi kifuani.

Mtoto wa wanandoa hao ameungua usoni, mikononi, tumboni na miguuni.

Pia Soma

Mama huyo amesema amekuwa akikumbana na vitendo vya ukatili kutoka kwa mwanaume huyo, ikiwa ni pamoja na kupigwa mara kwa mara.

Daktari wa hospitali hiyo, Hindi Mastai amesema hali ya mama na mwanaye inaendelea vyema licha ya mtoto huyo kutoweza kunyonya maziwa ya mama yake, kulazimika kumpa maziwa ya kopo.

Mmoja wa majirani wa mwanamke huyo, Epifania Kalolo anayemsaidia Mkami hospitalini hapo amesema mara kwa mara wanandoa hao wamekuwa wakigombana.

Kamanda wa polisi mkoani Dodoma, Gilles muroto alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mwanaume huyo anashikiliwa kwa mahojiano.

Chanzo: mwananchi.co.tz