Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mume, Mke Mahakamani kwa kumjeruhi Jirani yao

WhatsApp Image 2024 01 18 At 3.jpeg Mume, Mke Mahakamani kwa kumjeruhi Jirani yao

Thu, 18 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kesi inayowakabili wakazi wa Dar es Salaam, Bharat Nathwani (57), maarufu kwa jina la Chiku na mke wake Sangita Bharat Nathwani (54) inatarajiwa kuanza kusikilizwa ushahidi Februarri 19 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ambako wakituhumiwa kwa mashitaka manne likiwemo la kujeruhi na kutoa lugha ya matusi.

Wanandoa hao ambao ni raia wa Tanzania wenye asili ya India wanaoishi Mrima – Kisutu kwenye jengo la Lohana, Dar es Salaam walifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wa mahakama hiyo na kusomewa mashitaka yao na wakili wa serikali.

Katika hati ya mashitaka, washitakiwa hao wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne, ambayo wanadaiwa kuyatenda Julai 21,2023 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika shitaka la kwanza la kujeruhi linalomkabili Nathwani (Chiku) peke yake, anatuhumiwa kuwa Julai 21,2023 akiwa eneo la Mrima-Kisutu, jengo la Lohana ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam alimjeruhi jirani yake.

Nathwani anadaiwa kumsababishia madhara makubwa mke wa jirani yake, Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo ya saruji na kumjeruhi katika macho na sikio na kwa kumpiga katika shingo na kumsababishia maumivu.

Pia, katika shitaka la pili la shambulio la mwili linalomkabili Nathwani (Chiku) peke yake, tarehe hiyo na eneo hilo alimsababishia madhara kwa kumshambulia jirani yake Lalit Ratilal katika mwili wake kwa kumpiga ngumi na mateke kichwani.

Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu na la nne linalomkabili mke wake Sangita peke yake, ambapo anatuhumiwa kutoa matusi makubwa dhidi ya majirani zake, Lalit na Kiran kitendo ambacho kilileta fujo kwa namna ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani.

Kesi hiyo ilitakiwa kuanza kusikilizwa Jumanne mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Aaron Lyamuya, lakini ilishindikana kwa sababu hakimu huyo hakuwepo mahakamani kutokana na majukumu mengine aliyokuwa nayo.

Wakili wa Serikali, Frank Michael alidai juzi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga wa mahakama hiyo kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa na pia wana mashahidi wawili na wako tayari kuendelea.

"Mheshimiwa tunao mashahidi wawili na tupo tayari kuendelea, lakini tulikuwa tunaomba tarehe nyingine ya usikilizwaji kwa sababu hakimu anayesikiliza kesi hii hayupo," alidai Wakili Michael.

Hakimu Kiswaga aliwataka mashahidi hao kufika mahakamani hapo Februari 19,2024 kwa ajili ya kutoa ushahidi wao.

" Mashahidi nawataka mfike tarehe hiyo na huyo shahidi ambaye amesema tarehe hiyo hatakuwepo atawasiliana na wakili wa serikali atatoa ushahidi wake kwa njia ya mtandao 'Video Conference' kwa sababu vifaa vipo," alidai

Chanzo: www.tanzaniaweb.live