Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtunza vielelezo akwamisha kesi ya vigogo 11 wa TRL

Fri, 16 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa Mashtaka Katika kesi inayowakabili vigogo 11 wa Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL) ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kukiuka sheria wakati wa ununuzi wa mabehewa 25 umeshindwa kujibu hoja baada ya mtunza vielelezo wa Mahakama kuumwa.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Ijumaa Agosti 16,2019 kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kujibu hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi.

Awali, Upande wa utetezi ,Nehemia Nkoko aliiomba Mahakama hiyo  isipokee vielelezo vilivyowasilishwa na upande wa mashtaka ambavyo  ni michoro ya mabehewa ya kokoto iliyowasilishwa mahakamani hapo ni nakala ya kivuli badala ya nakala halisi na shahidi ameshindwa kuonyesha vitu gani vilivyopo kwenye hati ya makabidhiano.

“Ninaiomba Mahakama hii isipokee vielelezo hivi tumeona shahidi ametoa ushahidi wake kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) aliwakabidhi nakala ya kivuli ya michoro ya mabehewa ya kokoto badala ya nakala halisi na alipofuatilia alielezwa kuwa michoro halisi ipo wapi aliambiwa imechukuliwa na kamati ya awali iliyokuwa ikifanya uchunguzi,” alidai Nkoko.

Pia, shahidi huyo alipoulizwa vitu gani vilivyopo kwenye hati ya makabidhiano alishindwa kuonyesha mbele ya mahakama hiyo hivyo aliiomba mahakama hiyo isipokee vielelezo hivyo vitumike kwenye ushahidi.

Shahidi ambaye Kaimu Mhandisi Mitambo wa Shirika la Reli Tanzania(TRC), Albert Maganji  alidai Desemba Mosi,2015 akiwa ofisini kwake alipewa maelekezo kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu kuwa awape Takukuru michoro halisi ya mabehewa ya kokoto.

Pia Soma

Alidai michoro aliyowakabidhi Takukuru ilikuwa ni nakala ya kivuli na alipojaribu kufuatilia michoro nakala halisi ya mabehewa ya kokoto alielezwa ilichukuliwa na kamati ya awali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi ameahirisha shauri hilo hadi Agosti 28,2019 itakapokuja kwa ajili ya kujibu pingamizi hilo.

Vigogo hao wanaoshtakiwa ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu, Mkuu wa Kitengo cha Makenika na Mhasibu Mkuu Jasper Kisiraga, Kaimu Meneja wa Usafiri, Mathias Massae, Kaimu Mhandisi wa Ufundi na Meneja Ujenzi, Muungano Kaupunda na Mkuu wa Ufundi na Meneja Ujenzi, Ngoso Ngosomwiles.

Wengine ni Mhandisi Mkuu wa Ufundi, Paschal Mafikiri, Mhandisi Mipango Kedmo Mapunda, Kaimu Mhandisi wa Mawasiliano, Felix Kashaingili, Mkuu wa Usafiri wa Reli, Lowland Simtengu; Mkuu wa Ubunifu na Utengenezaji wa Nyaraka, Joseph Syaizyagi na Kaimu Mkuu wa Usafirishaji; Charles Ndenge.

Chanzo: mwananchi.co.tz